Baadhi ya
wazee wilayani Ludewa wamemuomba Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe
kuchukua fomu ya kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu mwaka huu na kudai
wamechoshwa na tabia ya kubadilisha viongozi.
Wakizungumza
mjini hapa wakati wa sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa Chama cha Mapinduzi
(CCM)iliyofanyika kijiji cha Nsele Kata ya Kilondo wilayani Ludewa, wazee hao
wamewataka wananchi katika jimbo la Ludewa kuendelea kumuamini mbunge huyo,
kwani hawaoni sababu ya kumbadili kiongozi ambaye bado wanaimani naye ya
kuendelea kuwaongoza.
Mwanasiasa mkongwe
wilayani hapa ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya
Ludewa, Mzee Hilali Nkwera alisema kuwa ni tabia iliyozoeleka kwa wananchi
kubadili viongozi kila kinapofika kipindi cha uchaguzi hali ambayo inarudisha
maendeleo ya wilaya nyuma.
“Katika
historia ya wilaya ya Ludewa ni mbunge mmoja pekee ndiye aliyewahi kudumu
madarakani kwa muda wa miaka 25 ambaye ni hayati Mathias Kihaule, lakini tangu
alipochukua utawala huo hayati Horace Kolimba (aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama
cha Mapinduzi) imekuwa ni desturi ya kubadilishana kila kipindi, hali ambayo ni
mbaya kwa maendeleo kwani mikakati ya kimaendeleo haiwezi kufanikiwa kwa muda
wa miaka mitano,” alisema Nkwera.
Alisema
mbunge Filikunjombe ameanza kufanya maendeleo kwa kasi kubwa hivi sasa katika
jimbo lake na wilaya ya Ludewa kwa ujumla, hivyo hapaswi kupingwa zaidi ya kuungwa
mkono kwa yale anayoyafanya kwani wananchi wa wilaya ya Ludewa hawana haja na
mtu mwingine wa kuliongoza jimbo hilo.
“Sisi kama wazee wa wilaya ya Ludewa hatuna
haja ya mbunge mwingine, wako vijana wanaokuja kutuomba tuwape nafasi na
tumewajibu wamuache mwenzao aendelee na mipango aliyoianza kuitekeleza ili
wilaya ibadilike zaidi tofauti na zamani, tumeamua kuacha tabia ya kubadilisha
wabunge kila mwaka kwani tumeziona athari zake za kurudi nyuma kimaendeleo”,
alisema Nkwera.
Akiunga
mkono kuhusu ombi la kutaka wananchi wawe na imani na Filikunjombe, Bi.Gerewada Nyandoa alisema kwa upande wa
wakina mama katika wilaya hiyo hawanashida na utendaji kazi wa Filikunjombe,
ambapo alisema ameweza kuwasaidia katika maendeleo ya ujenzi wa Zahanati ambazo
ni mkombozi kwa mwanamke hivi sasa katika wilaya hiyo.
“Kabla ya
ujenzi wa Zahanati, sisi wanawake tulikuwa tukipata taabu wakati wa kwenda
kupata matibabu, lakini toka alipochaguliwa mbunge Filikunjombe, jumla ya
Zahanati tatu zimeshakamilika na zinatoa huduma, hili ni jambo la kumpongeza
mbunge, tulikuwa tunatembea umbali mrefu kufuata matibabu,” alisema Nyandoa.
Alisema hivi
karibuni wazee wa kijiji cha Nsele Kata ya Kilondo walitoa fedha shilingi laki
moja na kumkabidhi Filikunjombe ili aweze kujiandaa kuchukua fomu ya kugombea
ubunge kwenye jimbo la Ludewa.
Kwa upande
wake, Mzee George Kilongo anayewakilisha wazee waliopo mwambao wa Ziwa Nyasa
aliusifia uongozi wa mbunge huyo katika kuwaletea maendeleo wananchi wake,
kwani ameweza kutembelea vijiji vyake vyote vya Ziwa Nyasa ndani ya miaka
mitano licha ya kuwa na Jiografia yenye milima na mabonde, lakini mbunge huyo
ameweza kufika vijiji vyote 77.
“Mfano vijiji vyenye mazingira magumu ya kufikika ni kijiji
cha Liunji,Kimata na Nkwimbili ambako hakuna mbunge ambaye aliwahi kufika,
lakini Filikunjombe ameweza kuvitembelea na kutoa misaada ya Afya,Elimu na maji
hali ambayo imewafanya wananchi wa vijiji hivyo kuona kuwa mbunge huyo anapaswa
kuendelea kuiongoza wilaya ya Ludewa kwa muda mrefu ili kuendelea kuwasaidia
wananchi,” alisema Kilongo.
Na Nyanda za Juu blog