PSPF WAJA NA MAFAO MAPYA


TAASISI ya Hifadhi ya jamii (PSPF), imeanzisha fao jipya linalojulikana kwa jina la Jenga ‘’Career’’ mkopo wa elimu, utakaonufaisha wanachama wake.

Akizungumza na kuwaelimisha wajumbe wa Baraza la Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Mkoa wa Mbeya, lililofanyika Jijini Mbeya jana, Afisa uendeshaji wa mfuko huo mkoa wa Mbeya, Daniel Herman, alisema wanachama wa mfuko huo wanaohitaji kusoma, watanufaka na fao hilo.

“Kwa kutambua umuhimu wa elimu katika jamii ya sasa, Mfuko wa PSPF umebuni huduma ya mkopo wa elimu kwa ajili ya wanachama wake kujiendeleza kielimu katika ngazi yeyote, iwe nje ya nchi na ndani ya nchi” alisema Herman.

Alisema mwanachama atakayenufaika na mkopo huo wa elimu ni yule takayethibitishwa na mwajiri na aliyechangia kwa miezi 24 tangu ajiunge na mfuko huo.

Mbali na mkopo huo wa elimu, afisa huyo aliitaja mikopo mingine mipya kuwa ni Jipange kimaisha ambao unawahusu waajiriwa wapya, mikopo ya ujenzi wa nyumba na mikopo kwa wastaafu ambayo ina masharti nafuu.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya, Alhaji, Mwangi Kundya, alisema elimu ni kama ua likaalo juu ya mmea, hivyo aliwasihi wakuu wa shule zinazomilikiwa na Jumuiya ya wazazi, kuwa wabunifu katika elimu ili wakosoaji wasipate mwanya wa kusema ikiwemo taasisi ya Haki elimu ambayo alisema ikiona mwanya ndiyo maana inaibuka na kukosoa.

Akizungumzia suala la Katiba Mpya, Alhaji Kundya, alisema kuwa, Serikali inapaswa kusambaza haraka nakala za katiba ili wananchi waweze kuisoma na kuielewa badala ya wananchi kubaki wanalishwa maneno na wanasiasa na kuyaamini pasipo wao hata kuisoma.

“Watu wanakariri anayosema fulani, sasa ni wakati wa serikali kusambaza nakala za katiba inayopendekezwa kabla ya maoni ili wananchi wapate fursa ya kupigia kura kile walichokisoma na wala siyo walichokisikia” alisema Alhaji Kundya