Ebola yatua Marekani

Ebola yatua Marekani

Mgonjwa wa kwanza wa Ebola Marekani
Mgonjwa wa kwanza wa ugonjwa hatari wa virusi vya Ebola amegundulika nchini Marekani, imethibitishwa katika mji wa Dallas, Texas.
Maafisa katika kituo cha afya cha Texas katika hospitali ya Presbyterian wamesema mgonjwa ambaye hakutajwa ametengwa katika hospitali hiyo.
Mgonjwa huyo anasemekana kuwa ni mtu anayeaminika kuambukizwa ugonjwa huo nchini Liberia kabla ya kuonyesha dalili za ugonjwa huo.
Zaidi ya watu 3,000 tayari wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola huko Afrika Magharibi na idadi ndogo ya wafanyakazi wa Marekani wa mashirika ya misaada wamepata nafuu baada ya kupelekwa kutibiwa Marekani.
Jumatatu, maafisa wa kituo cha afya cha Texas katika hospitali ya Presbyterian ya Dallas wamesema mgonjwa ambaye hakutajwa jina alikuwa akichunguzwa virusi vya Ebola na ametengwa katika hospitali hiyo.
Shirika la Afya Duniani, WHO limesema mpaka sasa zaidi ya watu 3,000 wamekufa kutokana na virusi vya Ebola, wengi wa waliokufa ni kutoka Liberia.
Nchini Nigeria, nchi yenye idadi kubwa ya watu barani Afrika kuna wagonjwa 19 waliothibitika kuugua ugonjwa wa Ebola na watu wanane wamekufa tangu mgonjwa wa kwanza kuthibitishwa nchini humo mwezi Julai..
Kuna mgonjwa mmoja aliyethibitika nchini Senegal, lakini hakuna taarifa za kifo mpaka sasa.
Ebola ni ugonjwa hatari wa virusi kuwahi kuzuka duniani.