Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa takriban watoto elfu tano nchini Liberia, Guinea na Sierra Leone, wamepoteza mzazi mmoja au wawili kutokana na ugonjwa wa Ebola.
Shirika
la umoja huo la kuwahudumia watoto, UNICEF, linasema kuwa kupata watu
wa kuwahudumia watoto hao imekuwa vigumu sana kwa sababu ya unyanyapaa
unaotokana na ugonjwa huo.Shirika hilo linasema kuwa baadhi ya watoto, wanalishwa na majirani, lakini wakati mwingi hawana watu wa kuwajali.
Kadhalika shirika hilo limetoa mfano wa mtoto mmoja mdogo mwenye umri wa miaka minne kuondokewa na wazazi wake wawili.
Mtoto huyo alikuwa anasaidiwa na mwathiriwa wa Ebola lakini mpango mzima huo ulikosa kufaulu hasa baada ya mtoto huyo kunyanyapaliwa na jamii nzima.
Watoto walipatikana wakiwa wametelekezwa hospitalini ambako wazazi wao walifariki au majumbani ambako ikiwa wana bahati wanalishwa na majirani zao ila kwa kutengwa.
''Maelfu ya watoto wanakabiliwa na hatari kubwa baada ya kuondokewa na mama au baba au familia nzima kutokana na Ebola,'' alisema afisaa mmoja wa shirika la Unicef Manuel Fontaine.
Idadi ya mayatima katika kipindi hiki cha Ebola ni wengi sana na idadi hiyo imeongezeka kulingana na ripoti nyingine zikisema kuna hofu kuwa huenda idadi hiyo ikaongezeka ifikapo mwezi Oktoba.
Unicef inasema kuna haja kubwa ya kuwepo mfumo wa kuwatunza watoto hao.