Maadhimisho yapita kwa kishindo Misri

Wafuasi wa jeshi wakiandamana medani ya Tahrir

Waandamanaji kadha wameuwawa katika mapambano yaliyotokea mjini Cairo na miji mengine ya Misri, wakati maandamano ya pande zinazopingana yamefanywa kuadhimisha mwaka wa tatu wa maandamano yaliyompindua Hosni Mubarak.
Mjini Cairo polisi walitumia moshi wa kutoza machozi na kufyatua risasi hewani kuwatawanya wanaharakati walioandamana na waandamanaji Waislamu wanaomuunga mkono rais wa zamani Mohamed Morsi ambaye alitolewa madarakani na jeshi.
Inaarifiwa kuwa bomu lilotegwa kwenye gari liliripuka karibu na kambi ya polisi katika mji wa Suez.
Wafuasi wa serikali piya walikusanyika katika medani ya Tahrir kuadhimisha siku hiyo, wakipiga kelele huku wamebeba picha za mkuu wa jeshi, Jenerali Abdul Fattah al-Sisi.