SHAHIDI wa tatu katika Kesi inayowakabili askari wawili na
Raia watatu ya unyang’anyi wa kutumia Siraha, Pasupuret Sreedhar ambaye ni raia
wa India na Mhanga wa tukio hilo ameiambia Mhakama jinsi washtakiwa
walivyofanikiwa kuwateka na kuwapora mali zao.
Akizungumza katika kesi hiyo huku akiongozwa na Wakili wa
upande wa Jamhuri, Basilius Namkambe mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya
Wilaya ya Mbeya, Michael Mteite, Shahidi huyo ambaye hakuweza kuzungumza
Kiswahili kabisa hali iliyopelekea Mahakama kumtafuta Wakili maarufu Mkoani
Mbeya, Sambwee Shitambala kuwa Mkalimani wake aliweza kuwatambua Watuhumiwa
wote watano.
Shahidi huyo aliiambia Mahakama hiyo kuwa Mnamo Januari Mosi
Mwaka huu aliwasili Jijini Dar Es Salaam akitokea kwao Nchini India akitumia
usafiri wa ndege wa Shirika la Oman akiwa na lengo la kufuatilia mradi wa
Uchimbaji dhahabu katika Migodi ya Chunya Mkoani Mbeya inayoendeshwa na kampuni
yao ya Otro Mining.
Alisema Januari 3,Mwaka huu alisafiri kutoka Dar es Salaam
kuja Mbeya akitumia Shirika la Ndege la Precision ambapo aliwasili majira ya
Saa Saba na Nusu Mchana na kupokelewa na rafiki yake Isaya Mkindi ambaye
walielekea naye moja kwa moja hadi Mbeya Hotel alikopata chakula cha Mchana.
Alisema baada ya hapo alipewa Dereva aliyemtaja kwa jina la
Ezekia ambaye alimpeleka Mwanjelwa kununua Mablanketi mawili kisha kurudi
katika Ofisi ya Rafiki yake huyo ambapo ilipofika majira ya Saa 10:45 jioni
walianza safari ya kuelekea Chunya akiwa na rafiki yake pamoja na dereva
Ezekia.
Alisema wakiwa njiani walipofika katika Milima ya Kawetere
kilomita 20 kutoka Mbeya Mjini walikuta magari mawili yakiwa yameachana kwa
mita 200 ambapo walilipita gari moja na ndipo walipokaribia gari lingine
wakakutana na vijana Wanne ambao mmojawapo aliwasimamisha na kuomba msaada wa
Spana ya kufungulia tairi ya gari yao wakidai kuwa inapancha.
Baada ya kueleza hivyo Wakili wa Serikali aliiomba Mahakama
imruhusu Shahidi huyo kama anaweza kuwatambua Watuhumiwa jambo ambalo
alitekeleza kwa kuwagusa Mshtakiwa namba moja, Tatu, Nne na Tano kisha
kuendelea na kutoa maelezo kuhusu kilichoendelea baada ya kuombwa spana.
Shahidi huyo aliendelea kusema kuwa baada ya Dereva wake
kuwajibu kuwa hawana spana ndipo Mtuhumiwa namba tatu ambaye ni Askari Magereza
alipotoka na kurudi akiwa na pingu mkononi na kumfunga Dereva kisha kumshusha
kwenye gari na kuelekea naye kwenye gari yao ndogo.
Aliongeza kuwa baada ya kufanya hivyo walimshika yeye huku
wakimuoneshea panga na kumwamuru asiongee neno lolote kisha kuhamisha mizigo
kwenye gari na kupeleka kwenye gari yao ambayo li Kompyuta za Mkononi mbili,
begi, mablanketi na Simu za Mkononi ambazo kabla hawajachukua alikuwa
ameshawasiliana na Mwenzie aliyoko Chunya aliyemtaja kwa jina la Jamir Amar.
Alisema akiwa ameshikwa na kuongeleshwa na watu hao simu yake
ilikuwa ikisikika na wenzie ambao waliweza kutoa taarifa katika Jeshi la Polisi
ambalo lilifanikiwa kuwakamata muda mfupi baada ya watu hao kutokomea na vitu
vyao na baada ya wao kuachwa akiwemo Dereva aliyekuwa amefungwa pingu kuachiwa.
Hata hivyo Wakili wa utetezi katika kesi hiyo Ladislaus
Lwekaza alimuuliza Shahidi huyo kama kweli aliwaona watuhumiwa wakiwa eneo la
tukio na siyo kalishwa maneno alijibu anawafahamu kwa sababu aliwaona wakifanya
tukio kwa sababu ilikuwa jioni kabla jua halijazima.
Wakili Lwekaza aliongeza kuwa akiruhusiwa kuwabadilisha
watuhumiwa mkao wao anaweza kuwatambua Shahidi huyo alijibu anaweza hivyo
akatakiwa kutoka nje ili waweze kuwachanganya ndipo awatambue jambo ambalo
lilipingwa na Wakili wa Serikali kuwa haijawahi kutokea utambuzi ukafanywa
wakati kesi inaendelea kusikilizwa na kuongeza kuwa jambo hilo hufanyika
kipindi cha upelelezi.
Kutokana na hoja hizo Hakimu Mteite alikubaliana na hoja ya
upande wa Mashtaka hivyo kutupilia mbali maombi ya upande wa mashtaka ya
kumtaka Shahidi atoke nje ili wamchanganyie watuhumiwa kwa ajili ya
kuwatambua na kuamuru kuendelea na
maswali mengine.
Watuhumiwa hao ni pamoja na Mshitakiwa namba moja ambaye ni
Askari Polisi PC James mwenye namba F8302 wa Wilaya ya Mbeya ambaye kabla ya
kufikishwa mahakamani alivuliwa Uaskari baada ya kuhukumiwa kijeshi.
Wengine kuwa ni mshtakiwa namba mbili kuwa ni Elinanzi
Mshana(22)Mkazi wa Iyela Jijini Mbeya, Askari Magereza mwenye namba B 500
Sajenti Juma Mussa(37) wa Gereza la Ruanda Mbeya,Mbaruku Hamis(29) Mkazi wa
Iyela na Amri Kihenya(38) Mkazi wa Iyela.
Akisoma mashtaka yao Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama
hiyo, Michael Mteite, Basilius Namkambe alisema watuhumiwa hao walitenda kosa
hilo Januari 3, Mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika eneo la Mlima Kawetere
barabara ya Mbeya Chunya.
Alisema watuhumiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa
kulizuia gari aina ya Pick Up lililokuwa likiendeshwa na Ezekia Matatira (34)
Mkazi wa Iyunga Jijini Mbeya ambaye alikuwa na mtu aliyekuwa akifahamika kwa
jina la Sreedhar Pasupelet(38) mwenye asili ya Kiasia wakitumia magari madogo
mawili ambayo ni GX 100 Toyota Cresta T 782 BEU na Gari linguine ambalo
lilikuwa na namba za Chesesi GX 6011832 aina ya Grand Mark II.
Hata hivyo Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 13, Mwaka huu
itakapoendelea tena kwa upande wa mashtaka kuwaleta mashahidi wake.
Na Mbeya yetu