HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI UFUNGUZI WA KONGAMANO LA
VIONGOZI WA DINI KUHUSU MATUMIZI YA RASILIMALI ZETU ZA GESI ASILIA, MAFUTA NA
MADINI KWA AMANI NA MAENDELEO YA TANZANIA,
WHITESANDS HOTEL, TAREHE 20-22 JANUARI 2014
Waheshimiwa
Viongozi wa Dini;
Waheshimiwa
Wakuu wa Mikoa;
Ndugu
Makatibu Wakuu;
Wageni
Waalikwa;
Mabibi na
Mabwana;
Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu,
mwingi wa rehema, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo
kujadili matumizi ya rasilimali zetu za gesi asilia, mafuta na madini kwa amani
na maendeleo ya nchi yetu. Kwa namna ya pekee nawashukuru viongozi wa dini kwa
kunishirikisha kwenye Kongamano hili muhimu na la aina yake. Mmenipa heshima kubwa ambayo
sikuitegemea. Asanteni sana.
Nawapongeza sana kwa uamuzi wenu wa busara wa
kuandaa Kongamano hili. Mmedhihirisha
kwa vitendo uhodari wenu wa kutekeleza jukumu lenu la msingi la kulea taifa
letu kiroho na kushiriki kikamilifu katika masuala mengine muhimu yahusuyo maendeleo
na ustawi wa Tanzania na watu wake. Ninyi
ni wazalendo wa kweli. Ni matumaini
yangu na ya Serikali ninayoingoza kuwa ubia wa aina hii utaimarishwa na
kudumishwa kwa faida ya nchi yetu.
Najua mlianza kwa kukereketwa na athari za
matumizi makubwa ya miti kwa matumizi ya nishati jambo ambalo linachangia sana
kuharibika kwa mazingira duniani.
Mmeishia kwenye Kongamano hili.
Lina uwiano kabisa kwani tunakata miti kwa ajili ya kuni na mkaa. Tukitumia gesi itatoa huko. Ni dhamira yetu hiyo.
Ndugu
Viongozi wa Dini;
Kongamano hili linafanyika katika kipindi mwafaka kabisa,
kipindi ambacho ugunduzi mkubwa wa gesi tayari umefanyika na dalili za
kugunduliwa zaidi zipo. Kipindi ambacho
hazina ya madini mbalimbali inazidi kugunduliwa na makampuni ya utafiti
yanatupa moyo kuwa mambo huenda yakawa mazuri zaidi. Pia, ni kipindi ambacho rasilimali zetu za
wanyamapori na misitu zinatishiwa kutoweka.
Ni kipindi ambacho wakulima na wafugaji na wafugaji na wahifadhi wa
misitu na wanyamapori wanashindania ardhi ya kufanyia shughuli zao. Sasa hivi ni kipindi mwafaka kabisa kukaa
chini na kutafakari jinsi gani rasilimali hizi zinaweza kulindwa na kutumika
kwa manufaa ya nchi yetu na watu wake wote zikiwanufaisha kule ambako
rasilimali hizo zipo na hata kule ambako hazipo.
Ni ukweli usiopingika kuwa Mwenyezi Mungu ameijalia
nchi yenye utajiri mkubwa wa rasilimali za asili. Ametujaalia ardhi kubwa yenye rutuba, madini
ya aina mbalimbali, misitu na mbuga za wanyama wa kila aina, hali ya hewa nzuri,
bahari, maziwa makubwa, mito mingi, watu wengi na kadhalika. Rasilimali hizi, kwa tabia yake, inatakiwa
zitumiwe vizuri ili kuboresha hali na maisha ya Watanzania wote sawia na kwa
miaka mingi na hata milele. Vinginevyo rasilimali
hizi zinaweza kugeuka kuwa chanzo cha mifarakano, magomvi na mauaji. Zinaweza kuwa balaa na kuleta maangamizi
nchini badala ya kuwa baraka na neema.
Mifano ipo ya nchi mbalimbali duniani zilizojikuta
zina migogoro na vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na kugombania utajiri
wao wa rasilimali za asili. Watu wa nchi hizo wanajuta kuwa na rasilimali
ambazo zimekuwa chanzo cha kuhatarisha amani, utulivu, usalama na hata uhai
wao. Kwa hapa Tanzania tunashukuru Mungu
rasilimali hazijageuka kuwa balaa na tunaomba hilo lisitokee. Tangu Tanganyika ipate uhuru na Zanzibar
kufanya Mapinduzi Matukufu na hatimaye nchi zetu mbili kuungana na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Serikali za awamu zote zimesimamia kwa makini rasilimali za nchi yetu ili
ziwanufaishe Watanzania wote. Tumetunga sheria
na sera mbalimbali kuhakikisha kuwa lengo letu hilo linatimia.
Hata hivyo, usimamizi wa sheria hizo na
utekelezaji wa sera zetu nzuri umekuwa unakabiliwa na changamoto mbalimbali kwa
nyakati mbalimbali. Mpaka hapa
tulipofika ni umahiri wa viongozi wetu ndiyo uliotuwezesha kuzuia mambo
yasiharibike na kugeuka kuwa matatizo makubwa.
Tumefanikiwa kiasi chake ingawaje hatujaweza kuzuia kabisa matatizo yasitokee
hapa na pale. Taarifa za kugombea
rasilimali zimekuwa zinasikika na nyingine zikiwa zimesababisha watu kupoteza
maisha, kujeruhiwa na mali kuharibiwa.
Tutafanya nini kukomesha hali hiyo isijitokeze, ni jambo ambalo sisi
kama taifa, yaani Serikali, wananchi na wadau mbalimbali, wakiwemo viongozi wa
dini hatuna, budi kulizungumza na kulipatia ufumbuzi.
Ndugu
Viongozi wa Dini;
Nimefarijika sana na uamuzi wenu wa
kufanya mkutano huu kuzungumzia rasilimali ya mafuta na gesi. Juhudi za kutafuta mafuta na gesi imeanza
tangu ukoloni, zikaendelea katika awamu zote baada ya Uhuru. Shirika la
Maendeleo ya Petroli (TPDC) lilianzishwa mwaka 1969 kuongoza juhudi hizo na kusimamia
sekta ya mafuta nchini kwa manufaa ya Watanzania wote. Hatujajaaliwa kupata mafuta mpaka sasa lakini
tumefanikiwa kupata gesi. Ugunduzi wa
kwanza wa gesi asilia ulifanyika Songosongo mwaka 1971 na baadae Msimbati,
Mtwara mwaka 1982. Utafutaji na ugunduzi
huo uligharimiwa na Serikali yetu na hivyo gesi hiyo ni mali ya Serikali. Baada ya ugunduzi huo makampuni binafsi
yalipata shauku ya kutafuta mafuta na gesi nchini.
Mwaka 1980 ikatungwa Sheria ya Utafutaji
wa Uzalishaji wa Mafuta kwa nia ya kuweka masharti na utaratibu wa makampuni
kushiriki katika utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi nchini. Pia unatoa mwongozo wa mgawanyo wa mapato
baina ya makampuni na Serikali. Sheria
hiyo imeendelea kufanyiwa maboresho kwa nyakati mbalimbali kulingana na
mahitaji ya wakati husika. Kuanzia mwaka
2007 shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia ziliongezeka kwa nguvu na
kasi kubwa. Juhudi hizo zilizaa matunda
mwaka 2010 kwa uvumbuzi wa kwanza wa gesi katika Bahari Kuu uliofanywa na
Kampuni za Orphir na British Gas. Baada
ya hapo ugunduzi umeendelea hadi kufikia futi za ujazo trilioni 46.5 za rasilimali ya gesi nchini mpaka sasa. Utafiti unaendelea na matumaini ya kupata
gesi zaidi yapo. Kufuatia ugunduzi huo,
Tanzania sasa ni moja ya nchi zimazohesabiwa kuwa na gesi nyingi duniani na ni
nchi inayovutia wawekezaji wengi katika sekta ya gesi. Kwa sababu hiyo, tukaamua kuifanyia mapitio
Sheria ya Utafutaji na Uzalishaji wa Mafuta na Gesi. Mwaka 2013 tumetunga Sera ya Gesi na
kurekebisha masharti ya Mkataba wa Kugawana Mapato yatokanayo na gesi
(Production Sharing Agreement) na kuongeza mgao wa Serikali.
Ndugu
Viongozi wa Dini;
Sera ya Gesi Asilia iliyopitishwa mwezi Oktoba,
mwaka jana (2013) imeeleza wazi, tena kwa lugha nyepesi, kuwa gesi ya Tanzania
ni mali ya Watanzania wote na itatumika kwa manufaa ya Watanzania wote – wa
kizazi hiki na kijacho. Katika matumizi
ya gesi, kipaumbele kitakuwa matumizi ya ndani.
Msingi wa hoja yetu ni ule ukweli kwamba ukiuza nje gesi yote, unapata mapato peke yake lakini unakosa faida
nyinginezo. Ukiitumia ndani unapata
mapato na faida nyingine nyingi, kwa mfano, uzalishaji wa umeme, matumizi ya
majumbani, kwenye magari na viwandani kuzalisha bidhaa mbalimbali. Hivyo basi
mnapoitumia ndani gesi inakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya nchi yetu.
Vilevile tupo katika mchakato wa
kuandaa sera ya kuwashirikisha zaidi Watanzania (Local Content Policy) ili
wanufaike zaidi na rasilimali yao ya gesi. Kwa sasa nimewaagiza TPDC wajiandae
kushiriki katika utafutaji wa gesi, uzalishaji wake mpaka inapofika sokoni. Wasiwe wagawaji vitalu tu pekee. Katika sera hiyo mpya pia tunaangalia
shughuli zinazoweza kufanywa na Watanzania ili tuone njia bora ya kuwawezesha
kushiriki. Kwa sasa tunadhani wanaweza
kushiriki kwa urahisi katika utoaji wa huduma kwa kampuni zinazofanya utafiti
na uzalishaji wa gesi na mafuta. Wapo
walioanza na wanafaidika. Nia yetu ni
kuona idadi yao inaongezeka.
Mabibi
na Mabwana;
Tumeanza pia mchakato wa kuiboresha TPDC ishiriki
katika uwekezaji kwenye sekta ya mafuta na gesi kwa niaba ya Watanzania. Katika utaratibu huo, baadaye TPDC itauza
hisa zake kwenye Soko la Mitaji ili Watanzania washiriki moja ka moja katika
kumiliki rasilimali hii muhimu.
Ndugu
Viongozi wa Dini;
Mambo yote hayo yanafanyika ili kuhakikisha
masilahi ya taifa yanalindwa na Watanzania wote wananufaika na rasilimali zao
kwa usawa. Changamoto kubwa tunayoiona
kuhusu ushiriki wa Watanzania kwenye utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi
ni uwezo mdogo wa fedha, utaalamu na teknolojia tulionao. Fedha zinazohitajika kwenye shughuli ya
utafutaji mafuta na gesi, kwa mfano, ni nyingi mno na Watanzania wenzetu
hawanazo na hakuna uhakika wa benki iliyo tayari kumkopesha mtu asiyekuwa
nacho.
Namna nyingine ni kuwapa maeneo ili wao watafute
wabia wawekeze. Lakini, mnapokuwa
mnasheria inayoshirikisha ubia baina ya Serikali na mwekezaji, kuamua kuacha
Serikali ili badala yake apewe Mtanzania binafsi si uamuzi rahisi sana
kuufanya. Mtu binafsi ananufaika
mwenyewe wakati Serikali inanufaisha wengi.
Ninachokiona nafuu kufanya ni kutumia mwanya wa ushiriki wa TPDC ili
tuone baadhi ya hisa ziuzwe kwa Watanzania.
Hapa kunakuwa na ubia wa TPDC na wananchi upande mmoja na Serikali
upande mwingine.
Jambo lingine tunalolifanya ni kuhakikisha kuwa
rasilimali ya gesi inatumika vizuri, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazo
vijavyo. Tutaanzisha mfuko maalum wa
kuhifadhi mapato ya gesi na kuwekewa masharti ya matumizi yake. Tutatunga sheria maalum kwa ajili hiyo na
tutafanya hivyo kwaka huu.
Mabibi
na Mabwaba;
Kwa upande
wa rasilimali ya madini mabadiliko makubwa ya kiuchumi yaliyoanza miaka 1980
katikati, Serikali ilijitoa katika uwekezaji na ikabaki kuwa mhamasishaji na
kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.
Kufuatia hali hiyo wawekezaji wengi walianza kuja kuwekeza katika maeneo
mbalimbali pamoja na utafutaji na uchimbaji wa madini. Serikali ikaweka Sera (1997) na Sheria (1998)
ya madini kusimamia sekta hiyo. Ni kweli
mapato ya Serikali na fedha za kigeni ziliongezeka kutokana na uzalishaji wa madini. Lakini palikuwa na manung’uniko mengi kutoka
kwa wananchi kuwa hawafaidiki sana na rasilimali zao.
Kamati mbalimbali ziliundwa
kuangalia tatizo lipo wapi ili jawabu lake litafutwe. Nilipochaguliwa kuwa Rais wa nchi yetu mwaka 2005 niliyakuta manung’uniko hayo na
kuamua tuyatafutie jawabu. Mwaka 2006
nikaunda Kamati ya Jaji Bomani ili ichambuwe mapungufu yaliyopo na kutoa
mapendekezo ya hatua za kuchukua.
Matokeo ya taarifa ya Kamati ile ni Sera Mpya ya Madini (2009) na Sheria
Mpya ya Madini (2010). Sera na Sheria hii inalenga kuongeza faida zaidi
kwa Serikali na jamii, bila kuwasahau wale wanaozunguka migodi.
Faida hizo ni pamoja na kuhimiza
kampuni za uchimbaji wa madini kufungamanisha uchumi kati ya sekta ya madini na
nyingine. Vilevile tumewataka waongeze
nafasi ya ajira kwa Watanzania na ununuzi wa huduma na bidhaa nchini. Aidha, tumeamua Serikali iwe inapata hisa
katika migodi mikubwa itakayoanzishwa siku za usoni. Ndiyo maana tunaendelea kufanya mazungumzo na
kampuni zitazochimba uranium na nickel.
Hatujamaliza lakini tunakwenda vizuri.
Halikadhalika, Sheria na Sera
vimeweka mkazo wa kuendeleza wachimbaji wadogo ambao ni Watanzania tu. Katika kutekeleza hilo, tumeanza kutenga
maeneo kwa ajili yao. Changamoto kubwa
inayowakabili ni ukosefu wa mitaji, vifaa na utaalamu. Kuhusu fedha, tumeanzisha mfuko wa kuwasaidia
na mwaka huu wa fedha tumewatengea jumla ya shilingi bilioni 2.5. Vile
vile tunakamilisha taratibu za kuanza kuwakodisha vifaa kupitia ofisi zetu za
madini za Kanda.
Jambo lingine kubwa ambalo
tunajiandaa kulifanya ili kunufaisha wananchi na nchi yetu ni kutunga Sheria
itakayohakikisha kuwa madini mengi yanayochimbwa nchini yanaongezewa thamani hapahapa
nchini. Hatua hii itachangia sana
kuongeza mapato na fursa ya ajira kwa watu wetu.
Nduvu
Viongozi wa Dini;
Nimeyasema haya yote kuwaonesha kuwa
Serikali haina mchezo katika usimamizi wa rasilimali zetu za asili. Tunafanya hayo kwa vile tunafahamu kuwa zinaweza
kutuletea maendeleo ya haraka. Lakini
pia zinaweza kusababisha nchi yetu kuingia kwenye dimbwi la migogoro
inayotokana na rasilimali. Yote mawili
yanaweza kutokea kutegemea tutasimamiaje na kuzitumiaje rasilimali zetu.
Jambo la muhimu ni kusaidiana kuelimisha jamii ya
Watanzania namna tulivyojipanga kusimamia rasilimali zetu za gesi asilia,
mafuta na madini. Waelewe kuwa utajiri
huu ni mali yao na hivyo ni haki yao kunufaika nao. Wafahamu kuwa ni wajibu wao kulinda na kuzitunza
rasilimali hizo ili zisipotee. Ninyi
mnayo dhamana ya kuelimisha jamii waelewe nia hiyo njema ya Serikali. Pia napenda kusema kuwa siyo kweli kwamba
Serikali haijali rasilimali za nchi au haitaki Watanzania wafaidike nazo; siyo
kweli eti Serikali inapendelea wawekezaji wageni kuliko wazawa na hakuna mkoa
au eneo linapuuzwa au kubaguliwa. Mimi
na Serikali ninayoiongoza tutakua watu wa mwisho kupuuza wazawa na kupendelea
wageni au kupuuza watu wa maeneo ambako rasilimali zinapatikana au
hazijapatikana.
Ndugu
Viongozi wa Dini;
Naomba muendelee kutekeleza jukumu lenu la msingi
la kulea taifa kiroho. Mhimize waumini
wenu wawe waadilifu na wazalendo. Waache
kujihusisha na vitendo viovu vya wizi, ubadhilifu, matumizi mabaya ya madaraka
na rushwa. Mkifanikiwa hilo, rasilimali
zetu zitakuwa salama. Vile vile
muendelee kuhubiri upendo miongoni mwenu, miongoni mwa waumini wenu na miongoni
mwa watu wote. Watu wakumbushwe kuwa
sisi wote ni viumbe wa Mungu na mbele yake sisi wote ni ndugu na inabidi
kuheshimiana na kuvumiliana kwa tofauti zetu.
Tukifaulu kwenye hili nchi yetu itabaki salama daima milele.
Nafahamu kuwa wapo baadhi ya watu ambao wanafanya
vitendo vya kuhujumu rasilimali zetu.
Wapo wanaoingia mikataba isiyozingatia maslahi ya taifa katika uvunaji
wa rasilimali zetu. Wapo wengine wanaokula
njama na wawekezaji ili Serikali ipunjwe mapato yake. Watu wa aina hiyo wapo katika jamii ye yote
ile na sisi kuwa nao si ajabu. Napenda mfahamu kuwa Serikali inapinga
vitendo vya aina yoyote vya kuhujumu rasilimali zetu. Ndiyo maana watu wa aina hiyo wanapobainika,
wanachukuliwa hatua na vyombo vinavyohusika.
Ninyi pia msichoke kuwafichua, wapo miongoni mwa waumini wenu.
Mabibi
na Mabwana;
Kabla ya kumaliza, napenda
kumshukuru Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospiter Muhongo na timu yake Wizarani
kwa kushirikiana na viongozi wa dini katika jambo hili muhimu. Naamini hatua hii ya kuwapa taarifa sahihi
viongozi wa dini kuhusu matumizi ya rasilimali zetu hususan gesi na madini
itasaidia kuongeza uelewa wa waumini wenu na wananchi kwa jumla. Watafahamu fursa zilizopo na jinsi ya
kuzitumia ili wafaidike nazo.
Nakushukuru pia kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa sera na mipango ya Serikali
katika sekta ya nishati na madini. Kazi
yenu nzuri inaonekana na sisi wote ni mashahidi.
Mwisho, nawashukuru viongozi wa dini
kwa kunishirikisha kwenye Kongamano lenu.
Naamini mkitoka hapa mtakuwa mabalozi wazuri wa kueneza ujumbe kuwa
rasilimali za Watanzania zipo kwenye mikono salama. Baada ya kusema hayo, napenda kutamka kuwa Kongamano la
Viongozi wa Dini kujadili matumizi ya rasilimali zetu za gesi asilia, mafuta na
madini kwa amani na maendeleo ya nchi yetu limefunguliwa rasmi. Nawatakia kila la heri na mafanikio katika
mwaka huu wa 2014.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.