Jeshi
la Polisi Nchini katika kuhakikisha linaendelea kutekeleza vyema
majukumu yake limekumbushwa kuchukuwa hatua za haraka za kudhibiti
ishara ya vitendo vya uvunjifu wa amani mara tu linapoanza kuona dalili
za muelekeo wa kuchezewa kwa amani ya Nchi.
Kauli
hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi wakati akizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Tanzania IGP
Ernest Mangu aliyefika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kushika
wadhifa huo mwishoni mwa mwaka uliopita.
Balozi
Seif alimueleza IGP Ernest Mangu aliyefuatana na Naibu wake Abdulrahman
Omar Juma pamoja na Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame
kwamba uchochezi ni jambo la hatari na kwa mujibu wa sheria na taratibu
za Nchi linatambulika kuwa ni kosa la jinai ambalo anapaswa muhusika
kuchukuliwa hatua za kisheria anapobainika kulifanya kosa hilo.
Alifahamisha
kwamba Serikali wakati wote isingependa kuona wananchi wake wanashindwa
kuendelea na harakati zao za kimaisha kwa sababu ya watu wachache wenye
tabia ya kuchochea uasi unaozaa vurugu zisizo na msingi wowote ule.
Alisema
kutokana na mabadiliko ya teknolojia ambayo pia hutumiwa vibaya na
wajanja wachache katika kufanya vitendo viovu askari wa jeshi hilo
wanapaswa kuwa makini katika kufuatilia vitendo vya baadhi ya watu
wanaotiliwa mashaka ndani ya Jamii.
Balozi
Seif alifahamisha kwamba hatua hiyo itafanikiwa vyema iwapo makamanda
wa jeshi hilo watapanga mikakati imara itakayosaidia kuimarisha zaidi
ulinzi kwenye maeneo yenye muelekeo wa kuibuka kwa vitendo hivyo.
“ Serikali isingependa kuona wananchi wanashindwa kuendelea na harakati zao za kimaisha kwa sababu tu ya watu wachache wanaochangia kushawishi vikundi vya kihuni kufanya vurugu katika maeneo yao “. Alisema Balozi Seif.
Akimpongeza
Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi Tanzania Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar alimuhakikishia Kamanda Ernest Mangu kwamba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kulipa ushirikiano zaidi Jeshi hilo
katika kuona linatekeleza vyema majukumu lililopangiwa na Taifa.
Mapema
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Ernest Mangu alimuhakikishia
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Jeshi la Polisi Nchini daima
litaendelea kulinda usalama wa raia na mali zao.
IGP
Mangu alifahamisha kwamba ulinzi huo utafanikiwa zaidi endapo
ushirikiano wa pamoja na wa karibu utakuwepo kati ya jeshi hilo,
Wananchi pamoja na viongozi wote, wa Serikali na Kisiasa.
Katika
uimarishaji wa jeshi hilo kiutendaji Kamanda Ernest Mangu alieleza
kwamba Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania tayari imekubali
kulidhamini jeshi hilo kwa kulipatia magari ili kupunguza changamoto
zinazolikabili jeshi hilo.
Wakati
huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alikutana na Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar Ndugu Johari
Masoud Sururu aliyefika Ofisini kwake Baraza la wawakikilishi Mbweni Nje
kidogo ya Mji wa Zanzibar kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa
rasmi kushika wadhifa huo Tarehe 24 Novemba Mwaka 2013.
Katika
mazungumzo yao Mkurugenzi huyo wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar Nd.
Johari Masoud Sururu alisema Idara hiyo katika kwenda na wakati
inatarajia kuanza kutumia Mtambo mpya wa Kisasa wa huduma za wasafiri
katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar.
Mkurugenzi
Sururu alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hatua hiyo
imekuja ili kujaribu kupunguza au kuondosha kabisa msongamano uliopo wa
wasafiri kwenye uwanja huo.
Alifahamisha
kwamba mpango huo pia utakwenda sambamba na Taasisi hiyo kuanza ujenzi
wa nyumba za wafanyakazi wake ili kukabiliana na tatizo la makazi ambalo
huleta usumbufu kwa watendaji hao.
Akimpongeza
Mkurugenzi huyo wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar Ndugu Johari Masoud
Sururu kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar aliuagiza Uongozi huo wa Idara ya Uhamiaji kuandaa utaratibu
makini utakaosaidia kudhibiti uvujaji wa mapato yanayotokana na uingiaji
wa wageni kwenye viwanja vya ndege na bandarini hapa Nchini.
Balozi
Seif alisema bado wapo baadhi ya watendaji wa Taasisi hiyo
wanaoonekana kutumia ujanja wakati wanaposimamia ukusanyaji wa mapato
yatokanayo na wageni wanaoingia Nchini.
Akizungumzia
suala la usalama wa nchi linalokwenda sambamba na wageni wanaiongia
Nchini Balozi Seif aliitahadharisha Taasisi hiyo ya Uhamiaji kuwa makini
na uingiaji wa wageni kiholela.
Alisema
wakati umefika kwa jeshi hilo kujiandaa kudhibiti watu au vikundi vya
watu vyenye ishara ya kutaka kuingia nchini kwa kujihusisha na vitendo
vyovyote vyenye muelekeo wa kuleta hujuma nchini.
“ Tumeshuhudia majirani zetu waliotuzunguuka ambao wamepatwa na misuko suko ya hujuma za uvunjifu wa amani, maafa na hata uharibifu wa mali za raia kutokana na kudharau baadhi ya vikundi vilivyokuwa vikijipenyeza ndani ya nchi hizo “. Alitahadharisha Balozi Seif.
Na ZanziNews