ANGALIA ALAMA HIZI


KUDUMU katika uhusiano kwa muda mrefu bila ndoa si kigezo kwamba mwenzi wako anakupenda. Tulia kwa muda, anza mwaka ukiwa na fikra mpya. Hebu jiulize, uko kwenye uhusiano na mwenzi wako kwa muda gani sasa?

Kuna dalili za kuingia kwenye ndoa? Marafiki, wanaotakiwa kujivunia kudumu kwenye uhusiano ni wanandoa. Ni halali kabisa kwa mtu aliye kwenye ndoa kutamba kwamba anafurahi kwamba yupo na mwenzake muda mrefu kwa sababu tayari wapo kwenye muunganiko.


Kwenye uchumba ni tatizo. Anaweza kukutumia (hata wanaume nao hutumika jamani) kwa miaka hata mitano au zaidi halafu baadaye akabadilisha mawazo – mkaachana!
Fikiri mara mbili. Ndiyo maana hapa kwenye All About Love nikakuandalia mambo ya msingi ya kuzingatia ili kutambua ukweli wa penzi lako kwa mwenzako.

Ni vizuri wakati ukiwa katika mwaka huu mpya, uwe na mtazamo mpya katika mapenzi. Hapa nachambua pande zote mbili; wanaume na wanawake. Nilianza na wanawake tangu wiki iliyopita ambapo nilieleza tabia za wanaume ambazo ni dalili mbaya kwamba, uhusiano huo hauna mipango ya baadaye. Hebu sasa tuendelee kabla ya kuhitimisha na kugeukia kwa wanaume.

Starehe kwa sana...
Mwenzi wa maisha anatakiwa kuwa na malengo ya baadaye kama tulivyoona kwenye vipengele vilivyopita.
Huyu ambaye hana malengo, utamgundua kutokana na tabia yake ya kupenda starehe kupitiliza. Hafikirii kabisa kuhusu maisha, muda wote anawaza starehe.

Wengi wa aina hii ni wale ambao bado wanaishi na wazazi au ndugu, wakiwategemea kwa kila kitu. Lakini pia kuna wengine ambao wanafanya kazi, lakini hawana malengo na kazi zao, muda wote ni starehe kwa sana.
Ni rahisi kukutana naye akiwa na pesa, lakini anapoishiwa kidogo hukukwepa. Anaogopa kwa sababu wewe kwake ni wa kujistarehesha tu.

Msiri sana
Hataki mambo yake yawe wazi, ukimwuliza anakuwa mkali. Hapendi uchunguze kuhusu mambo yake ya kazi, mbaya zaidi ni msiri hata kwa mambo ambayo una haki ya kuyafahamu.
Mathalani, simu yake inaweza kuingiza ujumbe mfupi wa maneno ambao utautilia shaka au akapigiwa simu na kwenda kuzungumzia nje, akirudi ukimwuliza kwa nini alitoka nje, anakuwa mkali. Huyu hana nia ndiyo maana haoni thamani yako.

Hataki ujue mambo yake, kwa sababu hajiamini. Ukweli ni kwamba kwa mtu mwenye sifa hii hawezi kuwa mwenzi wako. Ana umuhimu gani basi wa kuwa maalum kwa kiwango cha kufikiria atakuwa mwandani wako wakati ni msiri?

Kujali siyo kipaumbele...
Kwakuwa anakupenda kwa ajili ya starehe, ukiumwa au kupata tatizo ambalo utahitaji msaada wake, hatoi ushirikiano. Hawezi kukujulia hali wala kukusaidia kwa namna yoyote.
Hii inasababishwa na penzi lake ambalo siyo la kweli kwani yupo nawe kwa ajili ya starehe tu. Ikiwa ndivyo, bado unaendelea kumfikiria katika malengo ya maisha yako?

Yupo bize...
Mara nyingi amekuwa hataki mawasiliano, unaweza kumtumia meseji asikujibu na kama akijibu ni kifupi sana. Tabia hii ni mpya ambayo mwanzo hakuwa nayo! Ukimlalamikia, atakujibu kwamba yupo bize na kazi.
Kama ni suala la ubize, basi alipaswa kuwa nao tangu awali, lakini hilo ni kinyume chake, kwani ni tabia mpya ambayo inakushangaza. Ukiona alama hii, ujue kuna tatizo! Fikiria upya.

Hukupuuza...
Hapendi kukusikiliza katika suala zima la maisha yake, ukiachana na hilo pia, hapendi kukupa nafasi ya kutoa mawazo yako kuhusu jambo lolote lile! Mara zote, amekuwa akikuburuza kwa kila kitu.
Kama anakupenda, ni wazi kwamba angekupa nafasi ya kutoa mawazo yako kwa kila jambo linalohusu uhusiano wenu. Kukunyima nafasi hiyo ni sawa na kukuambia wazi kwamba, hana ‘future’ na wewe.
Mpenzi wako yupo hivi? Bado unafikiri kuna uwezekano wa ndoa tena hapo?

Kuachana ni wimbo
Hata kosa dogo tu, kwake ni kubwa na linatosha kabisa kukutishia kukuacha. Katika hali ya kawaida, kama anakupenda hawezi kukutishia kukuacha.
Mtu anapokosea huonywa na siyo kutishiwa kuachwa! Mpenzi ambaye kijiugomvi kidogo kinapotokea anakutishia kukuacha, ana matatizo na ni wazi kwamba hana nia.

Fikra mpya...
Vipengele hivyo bila shaka vimekupa mwanga mpya na sasa utakuwa makini katika uhusiano wako. Kama mpenzi wako ana alama hizo au baadhi yake, ujue ana matatizo na ni wazi kwamba hakupendi.
Ikiwa hakupendi ni wazi kuwa hutakuwa na sababu ya kuendelea naye maana anakupotezea muda wako bure. Ni suala la kufikiri na kuamua.
Wiki ijayo nitaendelea na mada hii ambapo nitageukia upande wa wanaume. Kaeni tayari, SI YA KUKOSA!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, All About Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani.