IDADI ya
wanachama katika chama cha Madibira Saccos imekuwa ikiongezeka kila mwaka kutokana na kuwepo kwa fursa mbalimbali za mikopo ikiwemo
ya kilimo ambayo imesaidia kubadilisha maisha ya wanachama waliowengi.
Akizungumza katika
mkutano mkuu wa kawaida wa 13 wa chama hicho,Mwenyekiti wa Madibira Saccos,
Athuman Kinyangasi alisema, kuwa idadi ya wanachama mpaka sasa ni 2613 na kuwa idadi hiyo ni ongezeko la wanachama
43 kwa mwaka huu.
Alisema kuwa
mbali na kuwepo kwa hamasa ya wananchi kujiunga katika chama hicho, pia chama
hicho kimekuwa mstari wa mbele kutoa fusa mbalimbali za mikopo ikiwemo ya
kilimo, Biashara, dhana za kilimo yakiwemo matrekta madogo na makubwa, mikopo
ya ujenzi wa nyumba, elimu, dharula, wajasiliamali, vijana na watumishi.
‘’Unajua
tunatoa mikopo mbalimbali katika chama chetu cha Madibira Saccos ili kuwezesha
wanachama mbalimbali kunufaika na mikopo hiyo hususani vijana ili waweze
kujiendesha pasipo kuilalamikia serikali kwa kila jambo,” alisema Kinyangasi.
Akitolea
mfano Mwenyekiti huyo alisema kuwa chama hicho kimekuwa makini kulejesha mikopo
kutoka katika Taasisi mbalimbali za kifedha yakiwemo mabenki na kuwa mpaka sasa
chama hicho kimesha rejesha kiasi cha sh milioni 200,000,000 pamoja na riba ya
sh 16,000,000 kutoka benki ya CRDB Iringa.
Kwa upande
wake Meneja wa Madibira Saccos Henry Mdapo alisema kuwa chama hicho kwa sasa
kimesha nunua hisa za 5000 zenye thamani ya sh 5,000,000 kutoka Benki ya
ushirika Tanzania.
Alisema
katika msimu huu wa fedha chama hicho kinatarajia kukopa sh.milioni 400,000,000 kutoka Baraza la Taifa
la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi kupitia Benki
ya CRDB –Iringa kwa lengo la kutoa fursa zaidia kwa wanachama kuchangamkia
mikopo ya kilimo.
Alisema
uamuzi wa chama hicho kuongeza fursa za mikopo ya kilimo kwa wanachama
kunalenga kuhakikisha wakulima wanalima na kuzalisha kwa tija zaidi kulingana
na vipaumbele vya serikali katika dhana ya kilimo kwanza.
Naye
Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi ya Madibira Saccos Said Kilawa alisema kuwa kamati
hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kusimamia fedha na mali zote za chama kwa
niaba ya wanachama,pamoja na pamoja na kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya
miradi ikiwemo mikopo kwa wanachama.
Ili
kuhakikisha chama hicho kinakuwa endelevu,Mwenyekiti huyo wa Kamati aliwataka
wanachama kuwawaaminifu katika kurejesha mikopo kwa wakati kwa lengo la
kuwawezesha wanachama wengine kunufaika na mikopo katika chama kwa maendeleo
yao.