Misaada ya dharura iliyokuwa imesubiriwa kwa hamu imeanza kupelekwa
katika eneo lililoathirika zaidi na kimbunga Haiyan nchini Ufilipino na kuwafikia
waathiriwa ambao wamekuwa wakiteseka kwa wiki sasa. Umoja wa Mataifa
umekadiria kuwa watu waliowachwa bila makaazi imefikia takriban milioni
mbili. Juhudi hizo za kusambaza misaada bado zimevurugika huku maafisa
wakisema manusura wa kimbunga hicho wanaendelea kuhangaika na kusubiri
chakula na maji . Ikiwa ni zaidi ya wiki moja baada ya Kimbunga Haiyan
kuwauwa watu 3,633, mamia ya wafanyakazi wa kimataifa wa misaada
wameweka hospitali za muda na kupeleka misaada. Mataifa kadhaa
yakiongozwa na Marekani yanaendelea kuwasilisha misaada yao kwa
wahanga wa janga hilo.