MIAKA 10 YA TCRA TANGU KUANZISHWA KWAKE

Meneja wa Mamlaka ya  Mawasiliano  Tanzania (TCRA) kanda nyanda za juu kusini  akizungumza na wadau mbali mbali wa mawasiliano katika kuadhimisha miaka kumi  ya TCRA tangu kuanzishwa  katika ukumbi wa Mtenda Sunset Hotel Soweto jijini Mbeya.Picha na Furaha Eliab


MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania kanda ya nyanda za juu kusini  imeazimisha miaka 10  tangu kuanzishwa kwake kwa kukutana na wadau  mbali mbali wa mawasiliano Mkoani  Mbeya kwa lengo la kubadlishana mawazo na kuelezea changamoto  na mafanikio katika sekta ya mawasiliano.
Akizungumza katika maadhimisho hayo meneja wa TCRA kanda ya nyanda za juu kusini Deogratius Moyo  alisema kuwa  watumiaji  wa simu za mikononi wameongezeka kutoka milioni  3.1 hadi kufikia takribani milioni 28.

Moyo alisema kuwa  idadi hiyo inafanya Tanzania kuwa na Wakazi  59  wenye simu kwa kila wakazi 100 na kwamba  utafiti uliofanywa na mamlaka ya mawasiliano kuna watumiaji wa wavuti wapatao milioni 7.5  ambapo idadi hiyo inaendelea kuongezeka.
Aidha Moyo amewataka wamiliki na mameneja wa radio  na Televisheni  kuhakikisha watangazaji wao wote wanazijua kanuni na sheria za mawasiliano na utangazaji ili kuepusha upotoshaji kwa jamii.
Alisema kuwa mamlaka hiyo inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwa ni pamoja na udhaifu hafifu wa maudhui kwenye televisheni,ukosefu wa miundombinu kutokana na miji mingi kujengwa holela na matumizi mabaya ya mitandai ikiwa ni pamoja na simu za mkononi.
Akizungumza kwa  niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Crispin Meela ameyataka makampuni ya simu kushirikiana katika uwekaji wa minara ili kuondokana na utitili wa  minara na kupunguza gharama  za matumizi ya simu kwa Wananchi.
Meela alisema kuwa utaratibu  wa hivi sasa unaofanywa na hayo makampuni  unasababisha uwepo wa utitiri wa minara,ongezeko la gharama kubwa kwa watumiaji na kuwepo kwa gharama kubwa katika kuweka minara hiyo.
Alisema kuwa utitiri wa minara hiyo unachangia kuwepo kwa matumizi ya fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika katika kuwasaidia wananchi kwenye shughuli mbali mbali za maendeleo.