KESI YA MAUAJI DHIDI YA PAPAA MSOFE YAPIGWA KARENDA

Marijan Abubakar  ‘Papaa Msofe’.
Kesi ya tuhuma za mauaji inayomkabili mfanyabiashara maarufu, Marijan Abubakar  ‘Papaa Msofe’ na mwenzake, imeahirishwa hadi Desemba 11 mwaka huu, kutokana na Wakili wa upande wa mashitaka kutokuwepo.
Kesi hiyo iliahirishwa  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Liwa.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka hakuwepo hivyo Hakimu Liwa alipanga tarehe nyingine.
Hakimu Liwa alisema kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa, kwa kuwa upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea.
Awali, upande wa utetezi waliiomba mahakama ifute kesi hiyo kwa sababu upande wa Serikali umechelewa kukamilisha upelelezi na washtakiwa wanateseka gerezani.
Katika kesi hiyo, Msofe na mfanyabiashara,  Makongoro Nyerere wanatuhumiwa kumuua kwa makusudi Onesphory Kituli. Washitakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo, Oktoba 11 mwaka 2011, nyumbani kwa Kituli, Magomeni Mapipa, Dar es Salaam.
Waliposomewa shtaka hilo, washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.