IRAN YASAINI MAKUBARIANO NA SHIRIKA LA IAEA

Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Usambazaji wa Silaha za Nyuklia, IAEA, na Iran zimesaini taarifa ya pamoja kuhusu ushirikiano wa siku za usoni kusuluhisha masuala yaliyosalia kuhusiana na mpango wa nyuklia wa Iran. Makubaliano hayo ni hatua muhimu kuelekea kuondoa wasiwasi wa shirika la IAEA kuhusu mpango huo na kuwafungulia mlango wachunguzi wake kuvitembelea vinu vingine viwili vya nyuklia; kinu cha Arak na kinu cha urutubishaji wa madini ya urani cha Gachin. 
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran akiwa na mkuu wa shirika la nguvu za atomiki la Iran, Ali Akhar Salehi, Mkurugenzi wa shirika la IAEA, Yukiya Amano, amesema makubaliano hayo yatafuatiwa na utekelezaji wa hatua muhimu katika miezi mitatu ijayo. 
Amano ameyaeleza makubaliano hayo kuwa hatua muhimu, lakini akasisitiza bado kuna kazi kubwa ya kufanya.