Umoja wa Ulaya umefanikiwa hivi leo kuanzisha makubaliano ya ushirikiano na Georgia na Moldova, lakini ukashindwa kuishawishi Ukraine, katika jitihada zake za kuimarisha mafungamano na mataifa sita, yaliyokuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Kisovieti.
Ukraine, ambalo ni taifa kubwa kabisa miongoni mwa hayo sita, ilikuwa tayari imeanzisha makubaliano ya kisiasa na kibiashara na Umoja wa Ulaya, lakini ilisita kuyasaini baada ya shinikizo la Urusi. Makubaliano haya ya leo na Georgia na Moldova nayo yanahitaji kusainiwa ili kuanza kazi rasmi, hatua inayotarajiwa mwakani.
Rais wa Lithuania, Dalia Grybauskaite amesema mwenzake wa Ukraine, Viktor Yanukovych, haonekani kuwa tayari kuendelea na mafungamano na Umoja wa Ulaya.
Rais wa Umoja huo, Herman Van Rompuy, amezipongeza Georgia na Moldova kwa ushujaa na dhamira zao za kisiasa.