Bunge la seneti nchini Italia
limepitisha hoja ya kumtimua Waziri Mkuu mstaafu wa Italia Silvio
Berlusconi katika bunge kutokana na kupatikana na hatia ya kukwepa
kulipa kodi.
Kufuatia hatua hiyo sasa Berlusconi anaweza kushtakiwa kutokana na kukosa kinga ya bunge.Berlusconi alijiondoa siku ya jumanne katika chama cha Forza Italia ambacho kipo ndani ya serikali ya mseto inayotawala nchi hiyo, hata hivyo serikali iliepuka kura ya kutokuwa na imani na kufanikiwa kupitisha bajeti.
Mjadala katika bunge la seneti umekuwa mkali ambapo maseneta kutoka pande zinazopingana wamekuwa wakitupiana maneno makali.
Manuela Ripetti kutoka chama cha Berlusconi cha Forza Italia alisikika akipaza sauti "Tunajua nia yenu ni kumwondoa Silvio Berlusconi".
Awali Berlusconi ambaye ametawala katika siasa kwa miongo miwili nchini Italia amewaomba maseneta kusogeza mbele kura hiyo ya kumwondoa kwa madai kwamba anao ushahidi unaothibitisha kuwa hajafanya kosa la kukwepa kodi.
na BBCSwahili