Na Baraka Mpenja, Mbeya
SHUGHULI pevu ya ligi kuu soka Tanzania bara msinu wa 2013/2014 inatarajiwa kuendelea kushika kasi wikiendi hii (Jumamosi na Jumapili) kwa mitanange ya kukata na shoka kushuhudiwa, ikizingatiwa kila timu inahitaji pointi tatu muhimu.
Hapo kesho Vinara wa ligi hiyo wenye pointi 14 kibindoni, Wekundu wa Msimbazi Simba, `Taifa kubwa` , wanaonolewa makali yao na winga machachari wa zamani wa klabu hiyo, kocha Abdallah Athmani Seif `King Kibadeni Mputa` watakuwa ugenini kukabiliana na Wapiga kwata wa Ruvu Shooting chini ya kocha Charles Boniface Mkwasa `Master` katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
Ruvu Shooting wao wapo nafasi ya 7 katika msimamo wa ligi kuu wakiwa na pointi 9 kibindoni na kesho wanahitaji ushindi ili kupanda juu zaidi.
Katika dimba la Azam Complex, maeneo ya Mbande, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam, Maafande wa nguvu ya soda, JKT Ruvu FC waliopo nafasi ya 6 na pointi 9 watakuwa kazini kuoneshana kibarua kizito na wana `Nkulukumbi`, Kagera Sugar waliopo nafasi ya pili na pointi zao 11.
Huko dimba la CCM Mkwakwani jijini Tanga, Wagosi wa ndima, Coostal Union waliopo nafasi ya 4 wakiwa na pointi 10 watapambana na Azam fc `Wana Lambalamba` kutoka jijini Dar es salaam. Matajiri hao wao wapo nafasi ya 9 na pointi 10 sawa na wagosi wa Kaya, lakini wanawazidi kwa wastani wa mzuri mabao ya kufunga na kufungwa.
JKT Oljoro waliopo nafasi ya 11 na mzigo wa pointi 5 watakuwa na kibarua kizito katika dimba lao la Sh. Amri Abeid kukwaruzana na wakali wa Juma Mwambusi, Mbeya City FC, waliopo nafasi ya 8 na pointi 8 kibindoni.
Baada ya mechi hizo za kesho, ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena jumapili (septemba 9) kwa mechi mbili kupigwa.
Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, klabu ya Yanga ya Dar es salaam waliopo nafasi ya 5 wakiwa wamejikusanyia pointi 9 watakuwa mwenyeji wa wakata miwa wa mashamba ya Manungu Turiani Mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar wenye pointi 7 katika nafasi ya 10. Mchezo huo utapigwa uwanja wa Taifa jijini Dar.
Na huko Mkwakwani Tanga, Mgambo JKT waliopo nafasi ya 12 wakiwa na pointi 5 kibindoni watakula sahani moja na Tanzania Prisons `Wajelajela` ambao wapo nafasi ya pili toka mkiani wakiwa na pointi 4.