YANGA VS JKT OLJORO: MBUYU TWITE NJE NAFASI YAKE KUCHUKULIWA NA JUMA ABDUL


BENCHI la Ufunda la Yanga limethibitisha kuwa beki Juma Abdul ndiye atakayecheza nafasi ya Mbuyu Twite.
 

Yanga ambayo inasaka pointi 10 kutwaa taji la Ligi Kuu Bara msimu huu huku ikiwa na mechi tano mkononi, leo itacheza na Oljoro JKT ya Arusha.
 

Mtanange huo utapigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, lakini itamkosa beki wake mahiri Mnyarwandwa Mbuyu Twite ambaye anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano.
 

Lakini, benchi la ufundi limesema pengo la kiraka huyo litazibwa vema na mlinzi wa kulia Juma Abdul.
 

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Felix Minziro alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa ni pengo kumkosa Mbuyu Twite katika mechi hiyo muhimu.
 

"Ni mchezaji muhimu kwetu. Lakini  imeshatokea hawezi kucheza kwenye mchezo huo, hivyo hatuna budi kumtumia mchezaji mwingine kucheza nafasi hiyo.
 

"Nafasi yake atacheza Abdul (Juma). Ni beki mzuri ambaye anajua majukumu yake. Tunaamini atacheza vizuri na kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri." alisema Minziro.
 

Pia, beki Juma Abdul alisema anaamini atacheza vizuri kulingana na maandaliizi ambayo wamefanya na kuhakikisha wanaibuka na ushindi kuzidi kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
 

"Tumefanya maandalizi mazuri. Kila mchezaji morali yake ipo juu. Kwa hiyo wategemee ushindi tu," alisema Abdul aliyetua Yanga akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro pamoja na Said Bahanuzi.

HABARI NA SHAFFH DAUDA