MARUPURUPU YA KUTOSHA UKIAJIRIWA ILEJE KAMA MTUMISHI WA HOSPITARI


IMEELEZWA kuwa watumishi watakao ajiriwa katika sekta ya afya wilayani Ileje Mkoani hapa watanufaika  na motisha itakayotolewa na Halmashauri hiyo kwa lengo la kuwavutia ili wasikimbie kufanya kazi katika wilaya hiyo.
 
Akizungumza na Mwandishi wa ELIMTAA mwishoni mwa wiki Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ileje Christopher Jakoracha alisema kuwa kutokana na upungufu wa watumishi katika sekta ya Afya ambao unatokana na watumishi wengi kuikimbia wilaya hiyo halmashauri imejipanga kuwapa motisha watumishi watakaokubali kufanya kazi wilayani humo.

 Jakoracha alisema kuwa baadhi ya mambo ambayo halmashauri imekusudia kuyafanya kwa watumishi hao ni pamoja na kuwalipa posho zao pindi wanapofika kwa ajili ya kufanya kazi, kitanda cha kulalia pamoja na godolo la kuanzia na chakula kwa siku atakazokuwa akisubiri mshahara wake wa kwanza.

 Aliongeza kuwa vitu vingine vitakavyotolewa ni pamoja na piki piki kwa ajili ya kurahisisha usafiri kwa mtumishi atakayepelekwa katika maeneo yenye miondombinu mibovu ili aweze kufanya kazi kwa uhuru na ufanisi zaidi.

 Mganga mkuu huyo alisema hadi hivi sasa tayari piki piki (5) ziko tayari na zimefika Halmashauri na nyingine (7) ziko kwenye bajeti ambayo inaishia mwezi wa sita hivyo aliongeza kuwa iwapo yote hayo yatatimizwa na ni dhahili kuwa watumishi katika halmashauri hiyo hawatoweza kuikimbia tena kama ilivyo hivi sasa.

 Kwa upande wake mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Sylvia Siriwa alisema kuwa changamoto inayoikumba Halmashauri hiyo ni watumishi kuikimbia katika kufanya kazi jambo ambalo alisema wameliona na wanataka kulitatua kwa kutoa vivutio kwa watumishi.

 Siriwa alisema kuna mikakati mingi ambayo baadhi yake hawezi kuiweka wazi kwa sasa ila muda ikifika ataiweka wazi ili jamii itambue na watumishi watakaletwa katika halmashauri hiyo wajue nini watanufaika wakiw wilayani humo.

 “Tumejipanga vizuri kuhakikisha watumishi katika sekta mbali mbali za halmashauri hii wasikimbie kufanya kazi na tutahakikisha kuwa mipango yetu inakwenda kama tulivyo panga ili watumishi waongezeke” alisema Siriwa na kuongeza.

 “Katika halmashauri hii tunaupungufu wa watumishi kwenye sekta ya afya kwa silimia 48 wakati kwenye sekta nyingine  inahitajika watumishi kwa asilimia 52 ili kuweza kukabiliana na changamoto zilizopo”

Aidha alisema kuwa hadi sasa kuna Zahanati tano ambazo hazina watumishi kabisa na hatujazifungua kutokana na tatizo hilo ikiwa ni pamoja na dawa lakini vile vile kuna zahanati zaidi ya tano ambazo nazo zitakamilika muda sio mrefu hivyo watumishi wanahitajika sana.