NUNDU: NINAPIGWA VITA



WAZIRI wa Uchukuzi, Omar Nundu amesema anapigwa vita na Naibu Waziri wake, Athumani Mfutakamba baada ya yeye kupinga Kampuni ya CCCC kupewa zabuni ya kupanua Bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini, Nundu amesema CCCC iliwahi kwenda kumshawishi yeye ili akazungukie katika nchi mbalimbali kutembelea miradi ya kampuni hiyo, lakini alikataa kwa vile alijua kuwa kufanya hivyo ni kama hongo.

Nundu amesema lakini cha ajabu, Naibu Waziri wake alipofuatwa na kampuni hiyo, alikubali na akapelekwa kwenye nchi za Mauritius, China na Guinea Bissau bila hata kumtaarifu bosi wake.

Amesema uhusiano wake na Naibu Waziri ulianza kuingia dosari wakati wa ujenzi la jengo la maegesho katika Bandari ya Dar es Salaam ambalo Nundu aliusimamisha baada ya kuona zabuni ya ujenzi wake hauna mashiko.

Aidha, Nundu amedai Mfutakamba aliwahi kumsemea yeye kwa Rais Jakaya Kikwete wakati alipotembelea Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kuwa anazuia mradi huo.

Amesema amekuwa mstari wa mbele kupinga miradi yote yenye dalili za rushwa, lakini baadhi ya watendaji ndani ya taasisi zilizoko chini ya wizara yake, wanamshutumu kuwa anaingilia maslahi ya mashirika hayo.

Kutokana na hali hiyo, Nundu asisitiza kuwa haoni sababu ya yeye kujiuzulu kwa kuwa hana kosa lolote amelolifanya na jambo analolitetea ni kwa maslahi ya nchi yake.

Amesema hana njaa ya kuiba fedha za umma, kwani kwa nafasi ambazo amewahi kushika tangu awe mtumishi sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi, ana fedha za kutosha za kuishi vizuri yeye na familia yake.