KUPIKIA SOKONO MARUFUKU


UONGOZI wa Soko la Mwanjelwa lililopo eneo la Sido jijini hapa wamewataka wafanyabiashara wanaojihushisha na upikaji wa vyakula(mama na baba lishe) sokoni hapo kutopikia chakula ndani ya eneo la soko hilo badala yake  wapikie  majumbani kwao ili kuepusha majanga ya moto yanayoweza kutokea.

Kauli hiyo imetolewa jana na Uongozi wa soko hilo ikiwa ni mara ya pili kutoa tamko hilo kwa wafanyabiashara hao,ambapo uongozi  huo ulidai kuwa machi 8 mwaka huu soko hilo lilinusurika kuungua tena na chanzo kikiwa ni kibanda kimoja cha mama lishe kushika moto licha ya kufanikiwa kuuzima moto huo mapema kabla haujasambaa.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara sokoni hapo Mwenyekiti wa soko hilo Charles White Syonga, alisema  kuwa mama na baba lishe walioko sokoni hapo wanatakiwa kutambua mambo ya msingi yanayoamuriwa na viongozi kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa soko hilo kwa lengo zuri la kujiepusha na majanga ya moto yanayoliandama soko hilo mara kwa mara.

Alisema kumekuwa na kasumba ya wafanyabiashara wachache wanaojihusisha na upikaji vyakula ndani ya soko hilo kutotii amri halali inayotolewa na uongozi wa soko, lakini wakati huu hawataweza kumvumilia yeyote atakayekaidi amri hiyo.

Aidha, Mwenyekiti huyo alitoa tadhadhari kuwa kwa yeyote atakayeonekana kutumia moto kwa namna yoyote ile, kama vile kunyoosha nguo kwa kutumia pasi ya mkaa, kuvuta sigara na wale wote wanaowasha ubani ndani ya eneo la soko hawatasita kumchukulia  hatua kali za kisheria.