AUWAWA KWA KUPIGWA NA WANANCHI

Wananchi mkoani Mbeya wameendelea kujichukulia sheria mkononi, baada ya mkazi mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Augustino (30), mkazi wa Igodima, Kata ya Iganzo, Jijini Mbeya ameuawa na wananchi wenye hasira kali baada ya kukutwa akiiba dukani.

tukio hili limetokea Aprili 12 mwaka huu majira ya saa 9:30 usiku, ambapo marehemu akiwa na wenzake wawili majina yao hayakuweza kufahamika mara moja walifungua duka la Grey Anangisye (35), mkazi wa Ilemi Darajani na kufanikiwa kuiba vitu mbalimbali.

Bidhaa hizo zilizoibiwa ni pamoja na mafuta ya kula lita 20, mafuta ya kupakaa, vocha za muda wa maongezi katika simu zenye thamani ya shilingi laki moja na vitu vingine mbalimbali ambavyo bei yake haikuweza kufahamika mara moja.

Marehemu Agustino alipoingia dukani akiwa na wenzake wawili walikurupushwa na muuza duka ambaye alikuwa amelala dukani hapo, kwa kupiga yowe ndipo majirani walipotoka na kufanikiwa kumkamata marehemu na kulazimika kuwataja wenzake.

Aidha baada ya marehemu kuwataja wenzake majina yao yalikabidhiwa kwa Mwenyekiti wa mtaa wa Iganzo Bwana Peter Mwamwaja na kuyapeleka katika Kituo cha Polisi kwa uchunguzi zaidi.

Hata hivyo baada ya marehemu kumaliza kutaja majina ya wqenzake, wananchi walianza kumpiga mtuhumiwa huyo na kisha kumchoma moto hadi mauti yalipomfika.

Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mbeya Barakiel Masaki amethibitisha kutokea kwa tukio hili na uchunguzi unaendelea na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya rufaa Jijini Mbeya.