CCM YAZIDI KUPOTEZA VIONGOZI KATIKA NGAZI YA VIJIJI MZIMU WA KUJUUZURU WAHAMIA MBOZI BAADA YA KUTOKA MBEYA MJINI

Wiki moja baada ya mfululizo  wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Jijini Mbeya kuachia nyadhifa zao kupitia Chama Cha Mapinduzi  (CCM) na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wimbi hilo sasa limebeba sura mpya kwa kuhamia Wilaya ya Mbozi.

 Katika hali isiyo ya kawaida Aprili 25 mwaka huu mchumi wa CCM wilaya hiyo Bi Happiness Kwilabya aliachia wadhifa huo na kujiunga na CHADEMA, akifuatana na wanachama 18 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Kata hiyo maarufu kama uwanja wa malori wilayani hapo.

Wanachama hao walipokelewa na Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya hiyo Bwana Joseph Mwachembe maarufu kama China, ambaye pia Katibu wa Mbunge wa Mbozi Magharibi Mheshimiwa David Silinde.

Akiongea katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi ambao umevuta hisia za watu wengi ambapo Bi Happiness amesema sababu kutoka CCM na kuhamia CHADEMA ni kutokana na mipango mingi inayopangwa si ya utekelezaji na badala yake wamekuwa wakijinufaisha wao binafsi na kuwafanya wananchi kuishi katika hali ya umaskini.

Aidha amezungumzia kero mbalimbali kuwa miradi mingi aliyokuwa akiibuni na kushauri kama mchumi imekuwa ikikwamishwa  na baadhi ya viongozi, ambao wapo kwa maslahi yao binafsi na si chama wala taifa kwa ujumla.

Hata hivyo amesema hajashawishiwa na mtu yeyote kukihama chama tawala na kwamba amehamia chama kingine ili kuhakikisha anapigania haki na maslahi ya watanzania.

Kwa takribani mwezi mmoja hivi sasa CCM imepoteza zaidi ya wenyeviti wa mitaa wapatao watano, ambao wameamia CHADEMA na mwingine aliposimamishwa kugombea wadhifa huo aliibuka na ushindi wa kishindo katika Mtaa wa Nonde Bwana Ezekiel King, ambaye pia alishawahi kuwa golikipa wa Tukuyu Stars na Mapinduzi Stars ya Mbeya, mtaa anaoishi Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Bwana Athanas Kapunga.