WATU watatu wamefariki dunia mkoani Morogoro katika matukio matatu tofauti liliwamo la mmoja kuchomwa na bisibisi wakati akiamulia ugomvi wa mke na mume .
Kamanda wa polisi mkoani hapa Adolphina Chialo amesema tukio hilo limetokea Machi 12 mwaka huu saa 5 usiku huko Tupendane Chamwino manispaa ya Morogoro.
Kamanda huyo alimtaja marehemu huyo Hoswin Alexzandra (37) mkazi wa Tupendane Chamwino ambaye alikwenda kuamualia ugomvi wa benald Kobero na mkewe ambaye hakuweza kufahamika mara moja jina lake, ambapo mume huyo aligeuza kibao na kuanza kumshambulia marehemu huyo na bisbisi hiyo ubavuni na mgongoni hali iliosababisha kuvuja damu nyingi na kufariki dunia papo hapo.
Amesema kuwa chanzo cha ugomvi wa wanandoa hao bado hakijajulikana , mtuhumiwa alikimbia baada ya mauaji hayo na polisi wanaendelea kumtafuta ili sheria ichukue mkondo wake.
Katika tukio la pili Mtu mmoja Amos Mondo (30) mkazi wa Changalawe Miombo wilayani Kilosa alifariki dunia baada ya kushindwa kuimudu baiskeli yake wakati akiwa katika mwendo kasi na hivyo kuanguka na kupata majereha kichwani.
Kamanda Adolphina amesema tukio hilo limetokea Machi 12 mwaka huu saa 4 usiku huko kijiji cha Masugu tarafa ya Masanze wilayani Kilosa ambapo marehemu huyo baada ya kuanguka alipelekwa hospitali ya wilaya ya Kilosa ambapo alifariki akiwa anapatiwa matibabu.
Katika tukio la tatu mfungwa mmoja Krispin Makao mwenye nambari 9 ya mwaka 2012 ( 35) mkazi wa Msowelo alifariki dunia akiwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro akisumbuliwa na ugonjwa wa Hypoghcaemiax .
Kamanda huyo alisema kuwa mfungwa huyo alifariki dunia Machi 10 mwaka huu saa 2 usiku katika wodi namba 9 hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro .
Alisema kuwa mfungwa huyo alikuwa akitumikia kifungo miezi 9 mkoani hapa baada ya kupatikana na hatia ya kosa la shambulio.