KATIKA hatua ya kushangaza baadhi ya waandishi wa habari wamezuiwa kufuatilia habari za mgomo wa wafanyabishara wa masoko baada ya kushushwa katika gari lililokuwa katika msafara wa Mstahiki Meya wa Halamshauri ya jiji la Mbeya,Athanas Kapunga.
Sakata hilo la kushushwa kwa waandishi wa habari waliopo katika mafunzo ya vitendo limetokea jana baada ya waandishi hao kuingia katika masafara wa Meya katika soko la Soweto,jijini Mbeya alipokuwa akipita kuzungumzia suala la mgomo wa wafanyabishara wa masoko mbalimbali ya Jiji la Mbeya.
Wakizungumza na gazeti hili mmoja wa waandishi Lwitiko Kaghubo kutoka Chuo cha Royal College of Tanzania Tawi la Mbeya ambaye yupo katika mafunzo ya vitendo katika kituo cha Radio cha Rock Fm alisema walifika katika soko la Soweto kuulizia uongozi juu ya msimamo wao wa mgomo wa kulipa ushuru mpya wa Sh.300 na kupandishiwa kodi.
Alisema baada ya kufika sokoni hapo ghafla walikutana na msafara wa Mstahiki Meya ambao ulifika bila taarifa na kuhitaji kukutana na wafanyabishara ambao hata wao walishangazwa na ujio wa Meya ambapo baada ya kuzungumza nao bila kufikia muafaka walilazimika kuingia katika msafara huo kuendelea kufuatili habari hizo katika masoko mengine.
Mwandishi huyo alisema baada ya kufika maeneo ya uhindini ambapo Meya alipenda kwenda kuzungumza na viongozi wa soko la muda la uindini lililopo maeneo ya Uwanja wa soka Sokoine ghafla Ofisa mmoja aliwaambia waandihi hao washuke kwani hawahitajiki katika msafara huo.
Alisema pamoja na kumweleza Ofisa huyo kuwa ni wanahitaji kuandika habari hizo ili umma uweze kujuwa kinachoendelea katika suala la masoko hakuweza kuwasikiliza jambo ambalo wanadai waliamua kushuka na kuacha msafara huo uendelee.
Mstahiki Meya,Athanas Kapunga alipotafutwa kwa njia ya simu na gazeti hili ili kuthibitisha tukio hilo simu yake iliita bila majibu pamoja na jitihada za kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Mbeya,Juma Idd aliomba samahani kwa tukio hilo endapo kweli limetokea na kudai yeye hayupo katika masafara huo lakini atawasiliana na Ofisa wake mmoja aliyepo katika msafara huo kujuwa kilichotokea.
Katika mkutano wa Soko la Soweto,Mstahiki Meya aliangusha lawama kwa wafanyabiashara kuwa kuishinikiza halmashauri kuboresha miundo mbinu ya masoko haraka bila kujali gharama za uboreshaji wa miundo mbinu na kuwataka wasioridhika na miundo mbinu iliyopo waipe muda Halmshauri wafunge masoko ili iboreshe miundo mbinu na baadae warudi kufanya biashara.
Kauli hiyo imewashtusha wafanyabishara wa masoko na kumuona Meya hakutumia busara katika kauli hiyo zaidi ya kutumia jazba huku wakidai watakaoumia siyo yeye baada ya kufunga biashara hizo bali ni wananchi walala hoi wanaotegemea huduma za soko hilo.
Mwenyekiti wa soko la Soweto,Ambele Mwandalima alisema walishangazwa na ujio wa ghafla wa Mstahiki Meya bila taarifa lakini hawataweza kukubaliana naye kutokana na Halamshauri kuwaahidi kabla ya kuwahamishia hapo kuwa watawasogezea na stendi ya mabasi ya abiri ya daladala jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa.
"Suala la Choo kweli Halamshauri imeshughulikia na barabara lakini tulipokuwa tumehamishiwa Soweto kwa sababu soko lipo kushoto yaani mbali na barabara walituambia wataiweka na stendi lakini tangu tumehamia hakuna wazo la kutuletea stendi na hali ya biashara ni mbaya,hivyo hatuwezi kulipa ushuru mpya hadi watukamilishie ahadi walizotoa,"alisema.