MAWAKALA wa pembejeo wilayani Njombe wamesema chanzo cha kusuasua kwa zoezi la ugawaji wa vocha za pembejeo za ruzuku katika maeneo mbalimbali nchini ni kutoka na serikali kutowalipa mawakala malipo ya msimu uliopita.
Aidha Serikali kupitia Wizara ya kilimo, chakula na ushirika imetakiwa kuharakisha ulipaji wa madeni ya fedha inazodaiwa na mawakala walio wengi ili zoezi hilo liweze kufanikiwa kwa asilimia 100 katika msimu wa kilimo unaofuata.
Hayo yamesemwa na Viongozi wa Chama cha mawakala wa Pembejeo wilayani Njombe (NAC),wakati wakizungumza na gazeti hili na kuongeza kuwa awamu ya nne ya mfumo wa vocha za ruzuku haukufanikiwa ukilinganisha na awamu tatu zilizopita ambazo zilifanya vizuri.
Mwenyekiti wa Chama hicho,Andrea Sanga alisema katika misimu iliyopita serikali iliwahisha mapema ugawaji wa vocha za pembejeo za ruzuku na fedha katika taasisi za fedha ambapo kufikia mwezi Septemba,Oktoba,na waliochelewa sana ilikuwa Novemba wakulima walio wengi walikuwa wameshapata pembejeo lakini katika msimu huu hadi mwezi januari vocha bado zinaendelea kutumwa.
"Kukiwepo na ugumu kwa kutolipwa mawakala fedha hata zoezi lenyewe litakuwa gumu kutekelezeka,wakishindwa kulipa kabla ya mwezi august serikali haitafanikiwa katika mfumo huu katika msimu unaofuata,'alisema.
Naye Mhasibu wa chama hicho,Sergius Mlowe alisema makampuni mengi sanjari na taasisi za fedha walisita kuwakopesha Mawakala kutokana na serikali kutoweka pesa hali iliyofanya zoezi kuwa gumu.