Serikali imewakaribisha wawekezaji kutoka China kuja kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya madini nchini.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ametoa wito huo Novemba 16, 2017 Jijini Dar es Salaam alipokutana na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Wang Ke na ujumbe alioambatana nao Wizarani kutoka kwenye Ubalozi huo ili kujadiliana masuala mbalimbali ya madini ikiwemo fursa za uwekezaji.
Waziri Kairuki alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za madini na hivyo zipo fursa lukuki za uwekezaji ambazo zinaweza kutumiwa na kampuni za nchini China kwa manufaa ya pande zote mbili.
“Rasilimali za madini ni nyingi na hivyo zipo fursa mbalimbali ambazo zinaweza kutumiwa na kampuni za China na wakati huo huo kuchangia katika uchumi na pato la Taifa kwa ujumla,” alisema Waziri Kairuki.
Waziri Kairuki vile vile alisema yapo maeneo ambayo wawekezaji wanaweza kushirikiana na Serikali ambapo alitaja baadhi yake kuwa ni uchimbaji wa madini kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), tafiti za utambuzi wa maeneo yenye madini kwa kushirikiana na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Chuo cha Madini (MRI).
Aidha, aliongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha madini yanayochimbwa nchini yanaongezwa thamani kabla hayajasafirishwa ili kukuza uchumi wa Taifa na wakati huo huo, kuongeza mapato ya Serikali na kuzalisha ajira zaidi.
“Madini yakiongezwa thamani hapa nchini, faida zitakazopatikana ni nyingi na ni kubwa ikiwemo ajira lakini pia mapato nayo yataongezeka kwa kuelewa thamani halisi ya madini husika,” alisema Waziri Kairuki.
Ili kufikia dhamira hiyo ya uongezaji thamani wa madini, Waziri Kairuki alisema Serikali ipo katika hatua za kuwapata wawekezaji mahiri wa kujenga viwanda vya kuyeyusha na kusafisha (smelting and refining) madini na alisema kuwa zipo baadhi ya kampuni kutoka China ambazo pia zimeonesha nia.
Mbali na hilo, Waziri Kairuki alisema Serikali imelenga kuwa na minada ya madini mbalimbali nchini na kwamba tayari upo mnada wa madini ya Tanzanite lakini lengo ni kuwa na minada pia kwa aina nyingine za madini ikiwemo Almasi na hivyo aliwakaribisha wafanyabiashara kutoka China kushiriki katika minada hiyo.
“Sasa hivi tunaelekea kwenye mnada wetu wa Tatu wa madini ya Tanzanite, tunawakaribisha kushiriki,” alisema Kairuki.
Alisema baada ya kufanikisha uanzishwaji wa minada itakayofanyika hapa nchini, katika siku za baadaye Serikali itaangalia uwezekano wa kuanzisha mnada kwa njia ya mtandao ambayo itamuwezesha mnunuzi kununua madini huko huko aliko kwa njia ya mtandao.
Vilevile, Waziri Kairuki alimuomba Balozi Ke kupitia ubalozi huo kuendeleza programu yake ya kuwajengea uwezo Watanzania kupitia masomo ya muda mfupi na mrefu hususan wafanyakazi kwenye Sekta ya Madini kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Uthaminishaji wa madini, Jiolojia, Jemoloji, Uongezaji thamani, Uhandisi migodi na Usimamizi wa Sekta ya Madini ili kuwa na wataalam wengi wenye uwezo mkubwa.
Aidha, Waziri Kairuki alimpongeza Balozi Ke kwa kuteuliwa kuwa Balozi wa kwanza mwanamke kuiwakilisha China nchini Tanzania na kumhakikishia ushirikiano wa dhati.
Kwa upande wake Balozi Ke alipongeza juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuwaletea wananchi wake maendeleo endelevu.
Alisema Serikali ya China itaendeleza ushirikiano wa karibu na wa dhati na Serikali ya Tanzania hususan kwenye Sekta ya Madini ili kuhakikisha sekta hiyo inaleta tija iliyokusudiwa kwa Taifa.
Alisema kampuni mahiri nyingi kutoka China tayari zimeonyesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya Madini na ziko tayari kuja kuwekeza Nchini.
|
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kulia) akijadiliana jambo na Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke. Picha na Na Mohamed Saif |