WAZIRI KAIRUKI ATANGAZA BALAA KWA WENYE VYETI VYA DARASA LA SABA SERIKALINI

Watumishi wa umma wenye kiwango cha Elimu ya darasa la saba wametakiwa kuwasilisha haraka Serikalini vyeti vyao vya kujiendeleza mpaka kidato cha nne vinginevyo watafutwa. Akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Temeke jijini Dar es salaam jana, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki alisema agizo hilo linawahusu watumishi walioajiriwa baada ya Mei 20, 2004.
Alisema watumishi walioajiriwa kabla ya tarehe hiyo wataendelea na nafasi zao na kama walijiendeleza wanahitajika kuwasilisha vyeti vyao kwa ajili ya kurekebishiwa taarifa. Waziri Kairuki alisema hatua hiyo inachukuliwa kama sehemu ya zoezi la uimarishaji wa mfumo wa serikali ambao utasaidia kupata taarifa sahihi za wafanyakazi na kupunguza ukubwa na gharama za uendeshaji.
“Waraka wa Serikali namba moja wa mwaka 2004 umetoa ufafanuzi, utaratibu kwa watumishi walioajiriwa serikalini kwa kiwango cha darasa la saba wanatakiwa kuwasilisha vyeti vyao vya kidato cha nne ili kukamilisha taratibu za utumishi wa umma,” alisema.
Aliwataka maafisa utumishi pamoja na ofisi za Makatibu Tawala kufanya kazi ya kuhakiki watumishi hao kwa mujibu wa Sheria na utaratibu wa kisheria. Alisema Serikali inaendelea kuhakiki taarifa za watumishi na imegundua baadhi ya taasisi za kiserikali zina watumishi wenye taarifa chafu.
Aidha, Waziri Kairuki alisema kuwa asilimia tano ya watumishi wana taarifa ambazo hazijakamilika.
“Utakuta mwingine ana jina moja, wengine vyeti vimekamilika lakini hayupo kwenye mfumo,” alisema. Amewataka Makatibu Tawala na maafisa utumishi kuhakikisha wanarekebisha haraka kasoro hizo pamoja na kuweka kumbukumbu sahihi za watumishi kuanzia siku waliyoajiriwa, elimu zao, michango ya hifadhi ya jamii na vyeo husika vya sasa.
Afisa Utumishi wa Manispaa ya Temeke, Mrisho Mlele, amesema kwamba watumishi 314 wameondolewa katika malipo ya mishahara. Alisema kuwa watumishi hao ni 270 waliobainika kughushi vyeti na 44 waliokuwa na vyeti vinavyotumiwa na watu zaidi ya mmoja. Aidha, alisema kuwa watumishi wengine 70 wanaendelea kuhakikiwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2u9xm6c
via IFTTT