SHAFFIH DAUDA ATANGAZA KUJITOA KWENYE UCHAGUZI WA TFF KWA TUHUMA ZA RUSHWA

Mtangazaji wa Clouds Media Group, Shaffih Dauda ametangaza kujitoa rasmi katika kinyang’anyiro cha kuwania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufuatia tuhuma za rushwa zinazomkabili.
Shaffih ambaye ni mmoja wa wachambuzi maarufu wa soka nchini ametangaza uamuzi huo mapema leo asubuhi Julai 28 wakati akizungumza kupitia kipind cha Clouds 360 kinachorushwa na Clouds Tv.
Akieleza sababu za uamuzi huo, Shaffih amesema kuwa imekuwa ni kazi ngumu ya miaka mingi kuweza kulijenga jina lake hadi kufikia hapo alipo leo, hivyo hawezi kuacha tuhuma hizo za rushwa zinazomkabili sababu ya uchaguzi wa TFF ziendelee kumchafua.
“Nimetumia muda mrefu kujenga brand yangu hakuna haja kuendelea kung’ang’ania. Suala la Rushwa ni kunichafua na mimi sitaki,” alisema Shaffih.
Uamuzi huu umekuja ikiwa ni siku chache tu tangu alipokamatwa na kuhojiwa na TAKUKURU yeye na wenzake kwa tuhuma za kupanga kufanya vitendo vya rushwa jambo ambalo alilikanusha vikali.
Shaffih alisema alikuwa kwenye kikao na viongozi wa soka Mkoa wa Mwanza, Mbeya na wengine wa jirani kwa sababu wanataka kuanzisha michuano ya Ndondo Cup katika mikoa hiyo, na si kweli kwamba walikutana kwa ajili ya suala la uchaguzi wa TFF.

from Blogger http://ift.tt/2vPKXhH
via IFTTT