MMILIKI WA VICHWA 13 VYA TRENI BANDARINI AFAHAMIKA

Wakati sakata la mmiliki wa vichwa 13 vya treni vilivyopo bandarini likiendelea kuumiza vichwa vya watu wengi, imeelezwa kuwa vichwa hivyo ni mali ya Shirika la Reli Tanzania (TRL) kwani wao ndio walioagiza kutoka kampuni ya Marekani.
Akiwa katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi kwa ajili ya upanuzi na ujenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema kuwa ana taarifa ya uwepo wa vichwa 13 vya treni bandarini hapo ambavyo mmiliki wake hajulikani. Rais alisema kuwa, mbali na vichwa hivyo kutojulikana ni vya nani, lakini inaelezwa kuwa ni vibovu.
Akizungumza, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko alisema kuwa vichwa hivyo vina nembo ya TRL na kwamba ulitokea mgogoro kati ya TRL na Kampuni iliyotengeneza baada ya kubainika kuwa mchakato mzima wa ununuzi haukuwa sahihi.
TRL ilinunua vichwa 15 vya treni kutoka Kampuni ya EMD ya Marekani na utengenezaji wake ukafanywa na Kampuni ya DCD ya Afrika Kusini.
Baada ya kusaini mkataba huo, Machi mwaka 2015 TRL ilipokea vichwa viwili vya treni na hivyo vilibaki vingine 13 ambapo ununuzi huo uligharimu Tsh 70.5 bilioni fedha ambazo zimelipwa na serikali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRL Machi 23, 2015, ununuzi huo wa vichwa vya treni ulikuwa ni mpango wa serikali wa kuifufua TRL chini ya mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Kufuatia TRL kuvikana vichwa hivyo kwa kile Rais Magufuli alichosema kuwa walidai hawajasaini mkataba, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imeiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) zitoe taarifa kuhusu vichwa hivyo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Edwin Ngonyani alisema kuwa taarifa zilizotolewa na Rais ni sahihi kwa sababu wizara haikuwa na taarifa kuhusu ununuzi huo ndio sababu akaziagiza TRA na TPA kufanya uchunguzi na kutoa taarifa kuhusu mzigo huo.
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2sLApNx
via IFTTT