MKUU WA MKOA WA DAR AIPONZA CHANNEL TEN

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limesema kwamba uamuzi wa pamoja wa kutotangazwa kwa habari zozote zinazomhusu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam bado haujatenguliwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa TEF, Neville Meena alisema kwamba msimamo wao bado uko pale pale hadi hapo uamuzi mwingine utakapotangazwa.
Meena alieleza kuwa TEF limethibitisha kutangazwa kwa habari za mkuu huyo wa Mkoa zaidi ya mara moja katika kituo cha runinga cha Channel Ten na mara moja katika tukio la msiba lililorushwa na kituo cha Redio cha EFM.
Pia, aliongeza kuwa imekuwa kawaida ya kwa vyombo vya kampuni ya Sahara (Star TV na Redio Free Afika) kutangaza habari za kiongozi huyo na kwamba kufanya hivyo ni kukiuka makubaliano ya ushirikiano wa kitaaluma (Professional Solidarity), hivyo uongozi unalifanyia kazi suala hilo.
Alisema kuwa uongozi wa TEF unawasiliana na taasisi husika na baada ya hapo itatolewa taarifa rasmi.
Meena alisema kwa sasa TEF inapenda kuwakumbusha wahariri wa habari kwamba makubaliano yaliyofikiwa kuhusu suala hili yako palepale hadi uamuzi mwingine utakapotangazwa.
“Tunaomba tuendelee kushirikiana katika kulinda uhuru wa taaluma yetu,” alisema.
Vilevile lifafanua kuwa mtu aliyefungiwa kutotangazwa habari zake ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na asiyo habari za mkoa huo.
“Hivyo basi siyo kweli kwamba kutotangazwa kwa taarifa zinazomhusu mkuu wa mkoa ni kutotangazwa kwa habari za mkoa. Huu ni upotoshaji unaofanywa kwa lengo la kuficha uovu alioufanya mhusika kwa kuvamia chombo cha habari usiku akiwa na silaha,” alisema Meena.

from Blogger http://ift.tt/2tiys0p
via IFTTT