MAPINDUZI YA DATA KUONGOZWA NA VODACOM

MKURUGENZI Mtendaji wa kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania, Ian Ferrao, amesema kampuni yake imejipanga katika kuwa kinara wa teknolojia ya data hapa nchini ili kuongeza idadi ya watumiaji wa mtandao huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Ferrao alisema katika miaka ya karibuni, idadi ya watumiaji wa data imeongezeka hapa nchini na Vodacom imejipanga vilivyo kutumia fursa hiyo.
“Katika miaka ya karibuni, Watanzania wengi zaidi wameanza kutumia vifaa kama vile simu na kompyuta kwa ajili ya kutafuta taarifa taarifa na maarifa mbalimbali yanayopatikana kupitia mitandaoni. Kwa sasa Vodacom inaona kuna fursa kubwa ya ukuaji katika eneo hili,” alisema bosi huyo wa Vodacom Tanzania.
Akieleza kuhusu hali ilivyo ya ukuaji wa watumiaji wa data, yaani matumizi ya internet kupitia simu za mkononi na kompyuta, Ferrao alisema katka kipindi cha miaka miwili tu, 2014/2016, idadi ya watumiaji wa data kupitia Vodacom imeongezeka kutoka watumiaji milioni 3.8 hadi watumiaji milioni 5.4; wote wakiwa watumiaji wa kudumu.
Akizungumza kwa kutumia takwimu, Ferrao alisema katika kipindi hicho kifupi, matumizi ya data yameongezeka kutoka asilimia 37 ya watumiaji wa simu hadi asilimia 44 kufikia mwaka jana.
Taarifa rasmi za Vodacom Tanzania zinaonyesha kwamba ongezeko kubwa zaidi la matumizi ya data liliongezeka katika kipindi cha mwaka 2014 na 2015 ambako ilitoka asilimia 37 hadi 43 ndani ya mwaka mmoja tu.
Ferrao alisema katika kujipanga kuongeza idadi ya watumiaji wa data, Vodacom Tanzania itaweka mambo mbalimbali yakiwamo bei rafiki kwa wateja na kuwa na kasi nzuri zaidi kuliko washindani wake.
“ Kuna njia kuu nne ambazo Vodacom Tanzania itazitumia katika kuhakikisha kwamba tunabaki kuwa vinara katika eneo la kutoa huduma bora na za kisasa kwa wateja wetu.
“ Kwanza ni wazi kwamba tutawekeza katika miundombinu yetu ili iendane na mahitaji ya watumiaji wa data waliopo Tanzania. Tutahakikisha watumiaji wa Vodacom wanapata data kwa spidi ya kuridhisha, kuwa na bei nafuu kwa wateja ndiyo mtandao wenye spidi nzuri ya internet kuliko mingine na pia kuweka sababu zitakazowafanya watu watake kutumia data zaidi,” alisema Ferrao.
Katika miaka ya mwanzoni ya matumizi ya simu hapa nchini, kampuni nyingi, ikiwamo Vodacom ilikuwa ikipata fedha nyingi kupitia watu kupiga simu kwa wingi na kutumiana ujumbe mfupi wa maneno (SMS).
Hata hivyo, tangu kuanza kwa matumizi ya data kwenye simu, takwimu zinaonyesha kwamba duniani kote, si Tanzania pekee, matumizi ya data yameanza kuwa makubwa zaidi kuliko hata watu kupiga simu na SMS kama ilivyokuwa zamani.
Tanzania ina fursa kubwa ya ukuaji wa matumizi ya data kwani uchumi wake umekua ukikua kwa wastani wa asilimia saba katika kipindi cha miaka kumi iliyopita huku ongezeko la watu pia likiwa la kuridhisha.
Tangu Vodacom imeingia hapa nchini mwaka 2000, imekuwa na kawaida ya kuwa ya kwanza kubuni vitu ambavyo baadaye vimekuwa vikiigwa na wengine.
Vodacom Tanzania ni kampuni tanzu ya kundi la kampuni za Vodacom lenye makazi yake nchini Afrika Kusini. Kampuni hiyo ya Afrika Kusini nayo ni sehemu ya kundi la kampuni za Vodafone lenye makao yake makuu nchini Uingereza.
Mwisho

from Blogger http://ift.tt/2u9Lusp
via IFTTT