MAHAKAMA YAWAMURU TIGO KUWALIPA MABILIONI MWANA FA NA A.Y KWA KUVUNJA SHERIA

Mahakama Kuu ya Tanzania leo Julai 21, 2017 imetupilia mbali rufaa iliyofunguliwa na Kampuni ya simu ya MIC Tanzania (Tigo) kupinga kuwalipa wasanii Ambwene Yesayah maarufu A.Y na Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA Tshs 2,185,000,000 kwa kutumia nyimbo zao bila idhini yaowala kuwa na mkataba.
Akizungumza na Swahili Times baada ya uamuzi huo wa mahakama, Wakili Albert Msando ambaye ndiye alikuwa anawawakilisha wasanii wao manguli wa muziki Tanzania amesema kwamba, huu ni ushindi muhimu kwa sanaa ya Tanzania.
“Mahakama imekubaliana na hoja zetu dhidi ya rufaa ya Tigo na kuitupilia mbali na kuamuru wasanii hao walipwe kiasi hicho kama kilivyokuwa kimeamuriwa mara moja,” alinukuliwa Msando akisema.
Awali, A.Y na Mwana FA walifungua kesi hiyo ya madai kwenye Mahakama ya Wilaya ya Ilala kupinga kitendo cha kampuni hiyo ya mawasiliano nchini kutumia nyimbo zao kwenye miito ya simu bila ya ridhaa yao au kuwa na mkataba.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Juma Hassan alitoa hukumu ya kesi hiyo Aprili 11, akiwapaushindi wasanii hao ambapo iliiamuru Tigo kulipa Tsh 2,185,000,000 kama faini ya jumla kwa ukiukwaji wa sheria.
Kampuni ya Tigo ilikata rufaa Mahakama Kuu ikipinga uamuzi huo wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, ambapo leo mahakama kuu nayo imetupilia mbali rufaa hiyo.
Wasanii hao wawili wameweka historia katika Sheria ya Haki Miliki nchini kwani ndio wasanii wa kwanza wa muziki wa kizazi kipya kufungua kesi ya hakimiliki na kushinda.
Kwa upande wake Mwana FA aliyekuwa mahakamani hapo wakati hukumu hiyo ikitolewa alisema kwamba, fedha hizo walitakiwa walipwe tangu hukumu ilipotolewa na mahakama ya wilaya, lakini ilishindikana kutokana na Tigo kukata rufaa mahakama kuu, na hivyo kutakiwa kusubiri maamuzi ya mahakama.
Aidha, alisema, kufuatia uamuzi wa mahakama kuu leo wa kutupilia mbali rufaa hiyo, wanatakiwa kulipwa fedha hizo katika kipindi cha muda mfupi.
Mafanikio haya makubwa katika kesi hii, huenda yakawachochea wasanii wengine ambapo kazi zao zinatumiwa kinyume na sheria kwenda mahakamani kudai haki yao. Lakini pia, uamuzi huu utaimarisha haki miliki za kazi za wasanii wa Tanzania.

from Blogger http://ift.tt/2gQf3y4
via IFTTT