FEDHA ZILIZOTENGWA KUJENGA OFISI ZA HALMASHAURI ZAAGIZWA KUJENGA HOSPITALI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma wilayani Momba kuanzisha mradi wa ujenzi wa hospitali.
Amesema sh. milioni 900 zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Halmashauri kwa sasa zianze kutumika katika kuanzisha ujenzi wa hospitali hiyo.
Agizo hilo alilitoa Ijumaa, Julai 21, 2017 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Tunduma.
“Kwa kuwa afya ni jambo muhimu katika utekelezaji wa kauli mbiu ya Rais Dkt. John Magufuli ya Hapa Kazi Tu, hivyo naagiza fedha zilizotengwa kuanza ujenzi wa ofisi zitumike katika ujenzi wa hospitali.”
Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa halmashauri hiyo kuongezea sh. milioni 126 katika ujenzi huo. Fedha hizo zilitengwa kwa ajili ya kuwafidia wamiliki wa eneo lililotengwa awali kwa ajili ya kujenga hospitali, ambapo aliwataka watafute eneo lisilohitaji fidia.
Pia, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) iandae ramani kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo na kuhusu suala la ujenzi wa ofisi Serikali italishughulikia.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya Mbunge wa jimbo la Tunduma, Mheshimiwa Frank Mwakajoka aliyeiomba kuiomba Serikali kuwajengea hospitali kwa kuwa halmashauri hiyo haina hospitali, hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi pale wanapohitaji huduma hiyo.
Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Bw. Juma Irando alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili wilaya hiyo kuwa ni ukosefu wa hospitali ya wilaya, ukosefu wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya na ofisi za Halmashauri.
Pia changamoto nyingine ni ubovu wa miundombinu ya barabara iliwemo ya Makamba-Ikana inayotakiwa kukarabatiwa inayounganisha ukanda wa juu na chini ili wananchi wa ukanda wa juu waweze kufika makao makuu ya wilaya.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wa wilaya ya Ileje baada ya kuwasili kwenye makazi ya Mkuu wa wilaya hiyo akiwa katika ziara ya mkoa wa Songwe Julai 22, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na wabunge Janet Mbene wa Ileje (kulia) na Juliana Shonza wa Viti Maalum baada ya kuwasili kwenye makazi ya Mkuu wa wilaya ya Ileje kuanza ziara wialyani humo Februari 22, 2017. (Picha na ofisi ya Wziri Mkuu). 
Baadhi ya watumishi wa umma, viongozi wa dini na taasisi binafsi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao mjini Ileje Julai 22, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa umma, viongozi wa dini na viongozi wa taasisi binafsi mjini Ileje Julai 22, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa jengo la hospitali ya wilaya ya Ileje akiwa katika ziara ya mkoa wa Songwe, Julai 22, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary (kushoto) wakitazama mbegu za mahindi zinazozalishwa na Kikundi cha SAM cha Ileje wakati alipotembelea banda la kikundi hicho kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara kwenye stendi ya mabasi ya Ileje Julai 22, 2017
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama vifaranga wa samaki wakati alipotembelea banda la Kikundi cha wanawake cha Tukazane cha Ileje kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara kwenye stendi ya mabasi ya Ileje Julai 22, 2017.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JULAI 22, 2017

from Blogger http://ift.tt/2vMWQE1
via IFTTT