WASIFU WA RAIS WA TANZANIA, DKT JOHN POMBE MAGUFULI

Maisha ya utotoni.
Jina lake kamili ni John Pombe Joseph Magufuli, kwa kabila yeye ni Msukuma na dini yake ni Mkristo. Alizaliwa Oktoba 29, 1959 Wilayani Chato Mkoa wa Kagera ambayo hivi sasa ipo Mkoa wa Geita.
Elimu
John Pombe Joseph Magufuli alianza elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Chato kuanzia mwaka 1967 na kuhitimu mwaka 1974. Baada ya hapo alijiunga na Seminari ya Katoke iliyopo Biharamulo kwa ajili ya elimu yake ya sekondari iliyoanza mwaka 1975 hadi 1977 na baadae akahamia Shule ya Sekondari Lake mwaka 1977 na kuhitimu 1978.
John Magufuli alijiunga na Shule la Sekondari Mkwawa iliyopo mkoani Iringa kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano na sita tangu mwaka 1979 na kuhitimu mwaka 1981 na mwaka huo aliohitimu akajiunga na Chuo cha Ualimu cha Mkwawa akasoma Diploma ya Ualimu katika masomo ya Chemistry na Hisabati.
John Pombe Joseph Magufuli (sasa Dkt na Rais wa #Tanzania), Shule ya Seminari Katoke, 1970s.
Mwaka 1988, John Magufuli alitunukiwa Shahada yake ya kwanza ya Ualimu akiwa amesomea masomo ya Chemistry na Hisabati kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) baada ya kuwa alijiunga chuoni hapo mwaka 1985. Mwaka 1994 John Magufuli alitunukiwa Shahada ya Uzamivu (Masters Degree) na mwaka 2009 akatunukiwa Shahada ya Umahiri (PhD) zote katika somo la Chemistry kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Rais John Pombe Magufuli akiwa mwanafunzi wa Shahada ya Umahiri ya Kemia (Masters Degree) katika Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam miaka ya mwanzo ya 1990.
Siasa na kazi
John Magufuli alijiingiza kwenye siasa kati ya mwaka 1982 na 1983 baada ya kuwa amefundisha kwa muda mfupi katika Shule ya Sekondari Sengerema mkoani Mwanza. Baadae aliacha Ualimu na kuajiriwa katika Chama cha Ushirika Nyanza kama Mkemia wa Chama hicho. Alifanya kazi hiyo kuanzia 1989 hadi mwaka 1995 alipochaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Chato kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ukiwa ndio uchaguzi wa kwanza tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi nchini.
Rais wa awamu ya tatu Mzee Benjamin Mkapa akimnadi Mgombea Ubunge Dkt Magufuli, jimbo la Biharamulo (East).
Baada ya kuingia Bungeni mwaka 1995 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi ambapo alitetea kiti chake cha ubunge mwaka 2000 na kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Ujenzi chini ya Rais wa Awamu ya Tatu, Mzee Benjamin William Mkapa.
Tarehe 4 Januari 2006 baada ya Rais wa Awamu ya nne, Dkt Jakaya Kikwete kuingia madarakani, alimteua John Magufuli kuwa Waziri wa ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kuanzia 13 Februari 2008 hadi 6 Novemba 2010, John Magufuli alikuwa Waziri wa Kilimo na Uvuvi, ilipofika 2010 aliteuliwa tena kuwa kuwa Waziri wa Ujenzi.
Mwaka 1995, Mama Anna Abdallah alimpokea na kumfundisha kazi kama Naibu Waziri wake wizara ya Ujenzi John Pombe Magufuli.
Mbio za urais.
Baada ya kuchukua fomu ya kutaka kugombea urais kama ulivyoutaratibu ndani ya CCM, Julai 15, 2015 John Magufuli alitangazwa kuwa mgombea wa urais wa CCM baada ya kuwashinda wapinzani wake akiwemo Asha-Rose Migiro, Amina Salum Ali, Benard Membe.
Katika mbio za urais, John Magufuli alikumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa mgombea wa CHADEMA, Edward Lowassa na baada ya wananchi kupiga kura Oktoba 25, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilimtangaza John Magufuli kuwa mshindi Oktoba 29, 2015 baada ya kujizolea kura asilimia 58% ya kura zote halali.
Dkt John Pombe Magufuli akila kiapo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Novemba 5, 2015.
John Magufuli aliapishwa kuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 5, 2015 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Urais.
Akitimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani, Rais Dkt. JohnPombe Joseph Magufuli amekuwa akigonga vichwa vya habari vya kitaifa na kimataifa mara kwa mara kutokana na kauli mbiu yake ya Hapa Kazi Tu. Rais Magufuli amejikita katika kupiga rushwa vita, kuhakikisha anabana matumizi ya serikali ili fedha hizo ziweze kutumika katika miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi au ukarabati wa viwanda.
Kutilia mkazo kwenye hilo, Rais Magufuli alifuta sherehe za sikukuu ya Uhuru, sherehe za sikukuu ya Muungano, amezuia viongozi wa umma kusafiri nje ya nchi bila kuwa ni kibali maalum, aliagiza kupunguzwa kwa gharama za sherehe ya ufunguzi wa Bunge, ameagiza mikutano na semina zifanyika katika kumbi za majengo ya umma.
Maisha binafsi.
Rais Magufuli ameoa mke mmoja, Janeth Magufuli ambaye alikuwa Mwalimu katika Shule ya Msingi Mbuyuni jijini Dar es Salaam na wana watoto watatu.
Dkt John Magufuli na mkewe Janeth Magufuli mwanzoni mwa miaka ya tisini.

from Blogger http://ift.tt/2sphQjX
via IFTTT