TAARIFA YA MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA (TFDA) KUHUSU MCHELE WA PLASTIKI

MAMLAKA ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imeunda kikosi maalum ili kupata ukweli juu ya mchele unaodaiwa kutengenezwa kwa kutumia plastiki baada ya picha kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa umeanza kutumiwa na baadhi ya mamalishe jijini Dar es Salaaam.
Baada ya picha hiyo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikielezea mchele huo kutumiwa na mamalishe kariakoo jijini Dar es Salaam, baadhi ya wananchi hususan wanaopata huduma ya chakula kwa mama lishe hao, walianza kuingiwa na hofu.
Mkurugenzi Mkuu wa (TFDA), Hiiti Sillo, alisema mamlaka imeanza kufuatilia suala hilo na kwamba imeunda timu maalum ili kubaini ukweli wa suala hilo.
Aidha, alisema taarifa za awali walizipata kupitia mtandano wa kijamii na Juni 8, mwaka huu, walitoa taarifa ya ufafanuzi kuwa hapakuwa na mchele wa aina hiyo ingawa wanaendelea kufuatilia.
“Mchele ambao upo na ambao TFDA tunautambua ni wa Basmati ambao huitwa Sunrice. Huu wa kutengenezwa kwa plastiki tunaendelea kufuatilia kama taarifa hizo ni za kweli au la,” alisema.
Alisema timu hiyo imeanza kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama ni kweli mchele huo uko sokoni. Aliwataka wenye taarifa za ziada kuhusu mchele huo wawapelekee ili kurahisisha uchunguzi.
“Tunaomba wenye taarifa za wapi mchele huu unauzwa, waliotumia watuletee au wapeleke taarifa serikali za mitaa wanakotoka, polisi au kwenye ofisi zozote za serikali ili tuweze kufuatilia jambo hili kwa urahisi,” alisema.
Mkurugenzi huyo alikiri kwamba mamlaka yake imepata taarifa juu ya mchele huo ingawa hadi sasa haijadhibitisha kama kweli umeshaingia nchini.
“Tayari nimeshatoa maelekezo kwenye kanda zetu za TFDA zikiwamo Mwanza, Arusha, Mbeya kuanza kufuatilia na ninavyozungumza ni kwamba ukaguzi unaendelea. Kama taarifa hizi ni za kweli tunamwomba huyu aliyetuma ‘clip’ (picha) hii kwenye mitandao ya kijamii ajitokeze ili atusaidie ni wapi alikula mchele huu maana clip inaonyesha mkono tu,” alisema.
Katika ‘clip’ hiyo, kijana huyo anaeleza kuhusu chakula hicho (wali) walioletewa na mama lishe huko Kariakoo huku akifinyanga tonge na kuonyesha tofauti yake na ule wa kawaida.
Sillo alisema taarifa mbaya zinazohusu chakula zinagusa watu na maisha yao kwa ujumla ndiyo maana wanamwomba mtu huyo awape ushirikiano ili wawajue wauzaji na wasambazaji.
“Wito wangu kwa watu wanaponunua kitu chochote wadai risiti hii itasaidia matatizo kama haya yanapojitokeza inakuwa rahisi kumkamata mhusika,” alisema.
Kuibuka kwa taarifa juu ya kuwapo mchele wa plastiki, kumezua taharuki na gumzo kwa wakazi wa Dar es Salaam ambao asilimia kubwa ndicho chakula chao na wengi hula kwa mama lishe.
 ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2sGACW9
via IFTTT