Nenda Ally Yanga, nenda, hakika jasho lako halitasahaulika kwenye jezi ya Yanga

NENDA Ally Yanga. Nenda Ally Yanga. Nenda Ally Yanga. Msinishangae kurudia kwangu kauli hiyo zaidi ya mara tatu. Soka limekumbwa na huzuni kubwa nchini. Kifo cha Ally Mohammed maarufu kama ‘Ally Yanga’ kimewagusa wengi sana. Haina jinsi acha iwe tu.
Kila nafsi itaonja mauti. Hakika kila mwanadamu lazima atarejea kwa Mola wake aliyemuumba. Hakika tumeumbwa kwa udongo na lazima tutarejea mavumbini kwa ajili ya kutimiza ufalme wa Mungu muumba. Hakika acha iwe tu, haina jinsi.
Abdul Dunia
Wadau wa soka nchini wamepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha shabiki ‘kindakindaki’ wa Yanga, Ally Yanga. Nenda tu kaka, haina jinsi. Ulikuja ukiwa Ally Mohammed na umeondoka ukiwa Ally Yanga. Umeondoka ukiwa kipenzi cha mashabiki wengi wa soka nchini.
Nenda tu Ally Yanga, nenda. Hakika jasho lako halitasahaulika kwenye wino wa jezi ya Yanga pamoja na timu ya Taifa ‘Taifa Stars. Halitasahaulika kamwe. Ulijitoa sana kwa ajili ya Yanga na Stars. Hakika hutasahaulika daima.
Ulikuja mtupu ila umeondoka na kitu Ally. Ulitokwa machozi kwa ajili ya Yanga na Stars. Ulifurahi kwa ajili ya Yanga. Kuna kipindi ulipigwa kwa ajili ya Yanga. Hakika Yanga itakukumbuka daima kwa uliyowafanyia.
Umejulikana na watu wengi kwa ajili ya Yanga. Ulitokwa jasho kwa ajili ya Yanga. Muda mwingine ulilia sana kwa ajili ya Yanga. Umefurahi kuipenda Yanga. Hakika umestahili kuitwa Ally Yanga. Haina jinsi, nenda tu kaka sisi sote tupo nyuma yako.
Kazi ya Mungu haina makosa. Ulikuja kwa kazi ya Mungu na umeondoka kwa kazi ya Mungu. Kwa hakika kazi ya Mungu haina makosa kamwe.
Ajali ya gari huko Mpwapwa mkoani Dodoma ilitafuta sababu tu, lakini Mungu pekee ndiye aliyepanga. Kazi yake Mungu haina makosa hata mara moja.
Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yako mahali pema peponi pia utukufu wake uwajalie nguvu na ustahimilivu familia yako na wapendwa wako wote.
Pumzika kwa amani Ally Yanga. Daima klabu ya Yanga na tasnia nzima ya soka nchini itakumbuka mchango wako katika soka kama shabiki mwandamizi.
Kuna wakati niliamua kumpa mkono kila nilipokutana naye baada ya mchezo wa Yanga ama Taifa Stars akiwa kajichafua na rangi za Yanga ama za jezi ya Taifa stars.
Niliwahi kutamani kukutana naye akiwa hana rangi zile za uwanjani lakini mpaka ameondoka sijabahatika kukutana naye akiwa bila rangi zile. Hakika alijulikana kutokana na rangi zile.
Ally alimvutia kila shabiki na mpenzi wa soka. Hakuwavutia watu kutokana na kuishabikia Yanga tu bali ubunifu wake jukwaani ulitosha kuwavuta watu wampende. Sio Mimi tu, sio wewe tu, hata kamera za runinga zilimfurahia kila timu yake ilipokuwa inashangilia goli.
Alivutia wakati wa kushangilia goli kwa staili ya kuchinja lakini pia alivutia zaidi wakati anahuzunika baada ya kufungwa. Ni watu wachache sana duniani wenye moyo kama Ally Yanga.
Namkumbuka Ally Yanga kwenye mechi kati ya Yanga na Simba mwaka 2011 pale kwenye Uwanja wa Taifa. Kichapo cha mabao 5-0 kilimchosha na kumtoa machozi kama mtoto aliyekuwa na njaa. Aina gani ya upenzi hii? Hiyo ndio maana halisi ya kuwa shabiki kindakindaki wa timu fulani.
Nenda ukapumzike Ally Yanga, picha zako ni ushahidi tosha wa ufalme wako jukwaani kwa jezi za Yanga na Taifa Stars katika Sanaa yako. Mwenyezi Mungu aipe faraja familia yako katika kipindi hiki kigumu. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. Amin.
Yanga yamlilia
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Salum Mkemi alithibitisha kwamba ajali hiyo imetokea na Ally alipoteza maisha kwenye ajali hiyo.
Ally Yanga atakumbukwa kutokana na mbwembwe zake kila Yanga ilipokuwa inacheza. Alipenda kujipaka masizi usoni huku akiweka kitambi cha bandia.
Wasifu wake
Jina lake kamili anaitwa Ally Mohammed maarufu kama Ally Yanga, alizaliwa Machi 1, 1984 mkoani Shinyanga. Ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto sita. Kabla ya umauti wake inafahamika alikuwa anaishi Yombo Vituka, Dar es Salaam.
Aliibukia Ubungo miaka ya nyuma kidogo ambako alikuwa anafanya shughuli ya kusajili laini za simu za mkononi katika vibanda vilivyokuwa pembeni ya kituo kikuu cha mabasi ya mikoani, Ubungo Terminal.
Ally Yanga alianza kuonekana kwenye Uwanja wa Taifa pamoja na kikundi cha mashabiki wa Yanga kilichojulikana kama Yanga Ubungo Terminal, ambako ndipo lilipokuwa tawi lake.
Tangu baada ya uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015, Ally Yanga aliadimika kwenye viwanja vya soka nchini kutokana na kujikita zaidi kwenye shughuli za Chama cha Mapinduzi CCM.
Ally hakuwa shabiki wa Yanga tu, enzi za uhai wake alikuwa akizishabiki pia timu za taifa, kuanzia za vijana na wakubwa za wanawake na wanaume. Hakika alikuwa mtu wa soka.
Alikuwa maarufu Afrika Mashariki kutokana na kwenda kuishabikia Taifa Stars kwenye mechi za Kombe la CECAFA Challenge zilizowahi kufanyika kwenye nchi za Kenya na Uganda.
Ally Yanga alikuwa akisafiri hadi nje ya Afrika Mashariki akiwa akiwa na Yanga na Taifa Stars kwenye mechi za kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia. Mungu ampumzishe kwa amani Ally Mohammed maarufu kama Ally Yanga. Amin.
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2tRsxep
via IFTTT