MFUNGWA AISHI KIFALME AKIENDELEZA BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA GEREZANI

Kamishna Sianga anasema vita dhidi ya usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya ni ngumu na hatari kuliko wengi wanavyoamini, na wakati mwingine wamejikuta wakihatarisha maisha yao.
“Tunapambana. Tunachofanya sasa ni kuhakikisha tunadhibiti na kuua kabisa mtandao wa waingizaji na wauzaji wa dawa za kulevya, na katika hili tunapata mafanikio makubwa,” anasema.
“Mpaka sasa tumewakamata mapapa 15 wanaojihusisha na uuzaji wa dawa hizo hapa nchini. Si kwamba tumefanikiwa kumaliza tatizo, lakini jamii inatakiwa kujua biashara hii ina mtandao mkubwa ni wa watu wenye pesa nyingi. Tumekamata hao 15 lakini kuna kundi jingine tena limeibuka.
“Yaani iko hivi, mkiwakamata hawa unaibuka mtandao mwingine. Kwa hiyo si kazi ndogo. Tunapambana sana kiasi kwamba tunatishiwa kuuawa.” Anasema wanaoendesha biashara hiyo ni watu wenye jeuri ya pesa.
“Nakumbuka wakati tunaenda kumkamata mmoja wa kigogo wa unga (alimtaja jina), alitaka kuonyesha jeuri ya pesa. Tulipofika kwake akawaambia vijana wake ‘wana njaa tu hao waulize wanataka shilingi ngapi?’,” anasema.
“Kinachoshangaza zaidi watu hawa wana mtandao ulioingia hadi ndani ya Serikali kwa maana kwamba wapo watu ndani ya Serikali wanafahamu shughuli zao na wanawalinda. Wengine ni wafadhili wakubwa ndani ya makanisa na kwenye jamii, wapo ambao ukitokea misiba kwenye jamii zao wao wanaubeba kwa kila kitu mpaka mazishi.
“Nilipomkamata muuzaji mmoja (anamtaja) baadhi ya viongozi wa dini na vigogo wa Serikali walianza kunipigia simu na wengine kunifuata ofisini wakilalamika kwa nini nimemkamata mfadhili wao na wengine wanakwenda mbali zaidi na kudai kuwa tumemuonea.”
Sianga anasema taarifa walizonazo muhusika mmoja wa dawa hizo ambaye alimtaja jina, alikuwa ni mfadhili mkubwa wa ofisi moja ya Serikali. Anasema mtu huyo alikuwa akigharimia matengenezo ya magari ya ofisi hiyo na kusomesha mpaka watoto wa watumishi wa Serikali. Anasema wakati mwingine hugharamia sherehe za harusi za watoto wa vigogo wanaomlinda na hata kuwalipia mahari.
Anasema kiongozi mmoja wa ofisi ya Serikali, ambaye alimtaja jina, alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakimlinda (muuzaji huyo) ili asikamatwe, hata juhudi za kumkamata zilipofanyika, alikuwa anavujisha siri.
Anasema muuzaji huyo wa dawa za kulevya, ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha maisha gerezani, anaishi gerezani kama mfalme.
“Tunapata taarifa kutoka gerezani kuwa anahudumiwa vizuri na inavyosemekana huenda wakati mwingine halali hata gerezani,” anasema. Kamishna wa masuala ya sheria wa mamlaka hiyo, Edwin Kakolaki anasema yupo mtu aliyefungwa kwa biashara ya madawa lakini anaishi gerezani kama mfalme na anaendesha biashara yake kama kawaida.
“Mbaya zaidi akiwa gerezani alinunua nyumba na watu wakachukuliwa kwenda kukaa katika nyumba ile kwa kazi moja tu ya kumpikia chakula.
Anasema nyumba hiyo hutumika kupikia chakula asubuhi na mchana kwa ajili ya mfungwa huyo wa dawa za kulevya na wakati anapoumwa, mkuu wa gereza huagiza apelekwe hospitali ambako pia huhonga ili alazwe hata wiki tatu.
Chanzo: Mwananchi
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2sWXH7S
via IFTTT