Jambo Moja Watanzania Waliloshindwa Kuelewa Mkutano wa JPM na Bosi wa Acacia

Kwa ufupi unaweza kusema kuwa wananchi walio wengi wameshindwa kuelewa mazungumzo ya kikao kilichofanyika kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzana, Dkt John Pombe Magufuli na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited Prof. John L. Thornton, Ikulu jana.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ilieleza kuwa, kampuni hiyo ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake hapa nchini.
Baadhi ya watu wengi wameonekana kuitumia sentensi hii pekee “kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza” bila kusikiliza kwa makini taarifa nzima ya kikao hicho.
Mazungumzo kati ya Rais Magufuli na kiongozi wa Barrick hayakumaanisha moja kwa moja kuwa Tanzania italipwa trilioni 108 ambazo kamati ilieleza kuwa taifa limepoteza tangu mwaka 1998 hadi Machi 2017 kutokana na kusafirisha kwa makinikia ya dhahabu kwenda nje ya nchi.
Taarifa hiyo iliendelea kueleza kuwa, Prof. John L. Thornton amesema kampuni yake ipo tayari kufanya mazungumzo na Tanzania yatakayozingatia maslahi ya pande zote mbili na pia ipo tayari kulipa fedha zote ambazo inapaswa kulipa kwa Tanzania.
Kwa upande wake Rais Magufuli alisema, serikali inakaribisha mazungumzo hayo na itaunda jopo la wataalamu watakaofanya majadiliano na kampuni ya Barrick Gold Corporation ili kufikia makubaliano ya kulipwa fedha zinazodaiwa na namna kampuni hiyo itakavyoendesha shughuli zake nchini maslahi ya pande zote mbili.
Kwa mantiki hiyo, kiasi cha fedha ambacho Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited itatakiwa kuilipa Tanzania kitataamuliwa na mazungumzo yatakayofanywa baina ya pande mbili.
Lakini mbali na mazungumzo hayo kuamua kiasi cha fedha ambacho Tanzania kitakacholipwa, itaamua pia njia bora ambayo kampuni hiyo itaendesha shughuli zake hapa nchi kwani kamati ilidai kwamba Acacia hawafanyi kazi kisheria na pia kuhakikisha kwamba rasilimali hizo zinanufaisha pande zote.
Vyombo vya habari hasa magazeti yameonekana kuripoti kwa namna inayoonesha kuwa Tanzania italipwa kiasi cha fedha (trilioni 108) kilichotajwa na kamati ya pili iliyowasilisha ripoti yake mbele ya Rais Juni 12 mwaka huu.
Baadhi ya vichwa vya habari vya magezeti ya leo vinasomeka, Barrick wamekiri kosa, wamesema wako tayari kulipa fedha tunazowadai (TanzaniaDaima), Acacia Kulipa (Nipashe), Acacia yasalimu Amri (Uhuru), Kampuni ya Barrick Yakubali Yaishe (HABARILEO).
Lakini, kuna uwezekano Acacia wakalipa fedha hizo, Tsh trilioni 108 ambazo kamati ilisema wameliibia taifa, kama taarifa za kamati zilikuwa ni sahihi na baada ya mazungumzo ya pande mbili wakaafikiana hivyo, lakini vinginevyo fedha hizo zinaweza kuwa nyingi zaidi au kuwa pungufu.
 ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2szdoBR
via IFTTT