Baada ya Kutumbuliwa Kwa Mara ya Pili..Profesa Muhongo Ashauriwa Kurudi Shule

MCHAMBUZI wa masuala ya siasa amemshauri aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini mpaka katikati ya wiki iliyopita, Profesa Sospeter Muhongo kuacha siasa na kurudi chuoni kufundisha elimu ya giologia baada ya kupata ‘ajali’ mbili za kisiasa ndani ya miaka miwili.
Profesa Muhongo alifukuzwa kazi na Rais John Magufuli Jumatano, ikiwa ni miezi 28 kamili tangu ajiuzulu nafasi hiyo Januari 24, 2015 chini ya Rais wa nne, Jakaya Kikwete.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benson Bana alisema baada ya miaka mitano ya ubunge wake ni vyema Prof. Muhongo akarudi kufundisha ambako atatoa uzoefu wa kuwa kiongozi serikalini na mwanasiasa.
“Hatima ya kisiasa amejijengea vizuri kwa kuwa wapiga kura wake wamemuelewa na wana imani naye ndiyo maana walimchagua,” alisema mchambuzi Prof. Bana. “Ataendelea kuwa mbunge mzuri wa jimbolake.”
“Lakini kwa misukosuko hii asipokuwa na roho ngumu anaweza kukata tamaa.”
Prof. Bana ambaye ni mtaalamu wa sayansi ya siasa, alisema kiongozi huyo bado ana nafasi ya kurudi kufundisha vyuoni kwa kuwa ni msomi mzuri wa miamba na madini na kwamba ameshajizolea umaarufu kwenye medali za siasa na kufahamika, ikiwamo uwezo wake kitaaluma.
“Kama mwaka 2020 Rais John Magufuli atapewa ridhaa ya kuendelea kuongoza, Profesa Muhongo hawezi kurudi tena kwenye uwaziri,” alisema Prof. Bana hivyo, akitafakari ni vizuri akarudi chuoni kutoa uzoefu wake wa serikalini na kuendelea na umahiri wake wa miamba na madini na kuachana na siasa.
“Siasa na madaraka ya uwaziri ameshaonja, machungu yake ameyaonja, abaki kuwa mshauri… aachane na siasa za leo ambazo ni ngumu sana.
“Kwa wasomi tumezoea kusema baibui ni baibui, lakini kwenye siasa ni tofauti.”
Prof. Bana alisema ni wazi hata hivyo kuwa wakati anaingia kwenye siasa, Prof. Muhongo alitegemea mambo hayo kwa kuwa siasa hazina adui wala rafiki wa kudumu.
“Aliingia kwenye siasa na kuaminiwa kwa kiasi kikubwa, akapewa nafasi kubwa serikalini kama ilivyokuwa kwa Profesa Anna Tibaijuka.
“Usomi ndiyo uzoefu wake wa muda mrefu, lakini kama tujuavyo siasa za nchi changa kama yetu unakuwa na madaraka ambayo wengi wanayapigania. Nirahisi kukuangusha kwa namna yoyote.”
Kwa upande wake Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alisema hatima ya Prof. Muhongo kisiasa itajukana baada ya kutolewa kwa ripoti ya uchunguzi wa kamati huru kwenye mchanga wa madini.
Alisema kwa sasa ni vigumu kuthibitisha kumhukumu mbunge huyo kwa kuwa changamoto ya kutonufaika kwa Tanzania katika madini yake ilisababishwa na mawaziri waliomtangulia wizarani hapo na kitendo cha serikali kuwasilisha bungeni miswada ya sheria za madini na nishati kwa hati za dharura na kupitishwa haraka bila wabunge kupata muda mwingi wa kuijadili.
“Kifo cha Prof. Muhongo kisiasa ni pale tu ikiundwa kamati huru ya kuchungumza mchanga wa madini na kubaini alihusika katika uzembe uliolisababishia taifa hasa ya matrilioni ya shilingi,” alisema.
“Kwa sasa ni vigumu kumhukumu kwa sababu makosa yalifanywa na mawaziri waliomtangulia na serikali ya CCM iliyotengeneza sheria za madini zinazonufaisha wawekezaji.”
WAPIGA KURA
Mhadhiri mwingine wa siasa UDSM, Dk. Bashiru Ally alisema bado Prof. Muhongo ana nafasi ya kwenye ulimwengu wa siasa kwa kuwa wenye kuamua hatima yake kisiasa ni wapiga kura wa jimbo la Musoma Vijijini.
Alisema kiongozi huyo amewajibishwa kwa uwaziri na siyo ubunge hivyo ataendelea kuwatumikia wananchi wake ambao wana imani naye.
Alisema mkataba wake na wananchi unaisha baada ya miaka mitano na hatima yake kisiasa iko mikononi mwa wapigakura wake kwa muda wa sasa na miaka ijayo kama atapenda kuendelea kuwatumikia.
Alipotafutwa na Nipashe jana kuzungumzia hatima ya Prof. Muhongo kisiasa, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema mwanasiasa mwenzake huyo bado ana nafasi ya kurejea kwenye Baraza la Mawaziri na hata kuwa kiongozi mkubwa nchini.
“Prof. Muhongo bado ana nafasi ya kusaidia nchi kama mbunge na anaweza kurudi kwenye Baraza la Mawaziri au hata nafasi kubwa zaidi ya hiyo. Mungu tu ndiye anajua mbeleni pakoje,” alisema Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini.
Nipashe pia ilimtafuta Katibu wa Wabunge wa CCM, Jasson Rweikiza, ambaye alisema Prof. Muhongo bado anayo nafasi ya kuitumikia nchi akiwa mbunge.
Alisema kuwa katika uchaguzi mkuu uliopita, mwanachama mwenzake huyo aliomba ubunge na si uwaziri.
“Lakini baada ya kupata uwaziri, Rais aliona anafaa kumpangia kazi nyingine zaidi, akaamua kumpa ili amsaidie lakini sasa Rais ameona kazi hiyo aliyompa, ameshindwa kuifanya na ameamua kumuondoa,” alisema.
Alisema kuondolewa kwenye uwaziri siyo mwisho wa safari yake kisiasa na haimuondolei ubunge wake kwa kuwa wapo wengi waliokuwa kwenye uwaziri na sasa wapo kama wabunge wa kawaida.
“Wapo wengi walikuwa kwenye uwaziri wakaondolewa kama Ezekiel Maige, Prof. Anna Tibaijuka na Andrew Chenge, na wengine wengi tu lakini wakagombea ubunge bila shida yoyote na wamepata,” alisema.
Rweikiza ambaye pia ni Mbunge wa Bukoba (CCM), alisema wananchi wa Jimbo la Musomo Vijijini walimpa ubunge Prof. Muhongo ili awatumikie na siyo uwaziri, hivyo anaweza kugombea na akarejea tena bungeni katika uchaguzi ujao wa mwaka 2020.
Naye Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile (CCM), alisema Prof. Muhongo bado anayo nafasi ya kurejea tena kwenye Baraza la Mawaziri kwa kuwa mchango wa utaalamu wake ni muhimu kwa taifa.
Alisema ubobezi wa Prof. Muhongo katika jiolojia ni muhimu si tu kwa Tanzania, bali duniani, hivyo mchango wake bado unahitajika katika maendeleo ya nchi.
“Sidhani kama huu ndiyo mwisho wa Prof. Muhongo kisiasa. Kumbuka katika uchaguzi uliopita, aliomba ubunge na si uwaziri,” alisema na kufafanua zaidi:
“Nafikiri sasa atakuwa na wakati mzuri zaidi wa kuwatumikia wananchi wa jimbo lake. Anaweza kugombea tena uchaguzi ujao na kurejea bungeni kisha kupewa nafasi nyingine ya kuitumikia serikali akiwa waziri.
“Ally Hassan Mwinyi alijuzulu uwaziri wa kutokana na vifo vya wafungwa na hivi karibuni tumeshuhudia mmoja wa mawaziri wa Ubelgiji akijiuzulu kutokana na shambulizo la kigaidi, Huko ni kuwajibika kutokana na changamoto iliyotikea.
“Prof. Muhongo bado anayo nafasi ya kuwania ubunge, kurejeshwa kwenye Baraza la Mawaziri na hata nafasi nyingine kubwa serikalini.”
TEGETA ESCROW
Kutumbuliwa kwa Muhongo kunakuja miaka miwili na miezi minne kamili tangu ajiuzulu nafasi hiyo kufuatia kashfa ya uchotwaji wa mabilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow, Januari 24, 2015.
Prof. Muhongo alimuandikia barua ya kujiuzulu Rais wa nne, Jakaya Kikwete akieleza nia yake ya kujiuzulu baada ya kujadiliwa na kuazimiwa bungeni, kwa sababu “nataka nchi isonge mbele”.
Dalili kwamba Prof. Muhongo angeondoka na matokeo ya uchunguzi wa kamati iliyoongozwa na Profesa Mruma zilikuja mapema Ikulu siku hiyo baada ya Rais Magufuli kumtaka ajipime.
“Ninampenda sana Profesa Muhongo, lakini pia ni rafiki yangu, lakini kwenye hili ajifikirie! Aji-asses (ajitathimini) na bila kuchelewa nilitaka aachie madaraka,” alisema Rais Magufuli akionekana mwenye huzuni.
Muhongo ni Mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini kwa tiketi ya CCM, ambaye alichaguliwa mwaka 2015.

from Blogger http://ift.tt/2qysT7y
via IFTTT