WAKATI Bunge la Bajeti likianza leo Dodoma, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kitendo cha wabunge kukaa bungeni kwa miezi mitatu kujadili Bajeti ya Mwaka 2017/18 ni sawa na kupoteza muda.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini alidai jana kuwa bajeti hiyo ya Sh trilioni 31.6 haiwezi kutekelezeka, akirejea alichokiita uongo wa utekelezaji wa Bajeti iyobakiza miezi mitatu kumalizika, akisisitiza kuwa ya sasa haitatekelezwa zaidi ya Sh trilioni 28.
Aliwataka wabunge kuhoji utekelezaji wa Bajeti ya 2016/17 na kutaka ichambuliwe kwa kina kuonesha hali halisi na kuitaka Serikali iandike upya Bajeti inayopendekezwa ya mwaka 2017/18.
“Wabunge wasikubali matumizi ya kawaida kuitwa ya maendeleo. Mfano, mwaka huu ili kuonesha Bajeti ya Maendeleo ni kubwa, Serikali imerundika matumizi kama kununua dawa, fedha za ruzuku zinazokwenda shuleni na maeneo mengine na kuziita za maendeleo,” alisema.
Alitoa kauli hiyo takribani siku tano tangu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Katika maelezo ya Dk Mpango, Serikali ilitoa theluthi moja tu ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mwaka 2016/17 huku mwaka ujao wa fedha ikipanga kukusanya na kutumia Sh trilioni 31.6 ikilinganishwa na Sh trilioni 29.5 za Bajeti ya mwaka huu, huku uwiano wa bajeti ya maendeleo ukishuka hadi asilimia 38 kutoka 40 ya mwaka jana.
Dk Mpango alisema hadi Februari mwaka huu, fedha zilizokuwa zimetolewa kwa ajili ya maendeleo ni Sh trilioni 3.97 kati ya Sh trilioni 11.8 zilizopitishwa na Bunge Juni mwaka jana, kugharimia miradi ya maendeleo.
Katika taarifa yake aliyoituma kwa vyombo vya habari jana, Zitto alisema: “Ni dhahiri Tanzania inakwenda kupoteza muda wa miezi mitatu kujadili Bajeti nyingine ambayo ni ya kujidanganya. Bajeti halisi ya 2017/18 haitazidi Sh trilioni 28. Tulisema kwenye Bajeti ya 2016/17.”
Kwa mujibu wa Zitto, bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano (2016/17 ) imeonesha upungufu mkubwa katika utekelezaji na kwamba baada ya kupitia taarifa zilizowasilishwa na Dk Mpango kwenye kamati za Bunge za kisekta, alibaini kuwa Bajeti ya 2016/17 ilipaswa kuwa Sh trilioni 24.8 na si Sh trilioni 29 iliyowasilishwa na Serikali Juni mwaka jana.
“Mpaka Machi, lengo la makusanyo ya mapato yote ya Serikali limeshindwa kufikiwa kwani ni asilimia 79 ya makusanyo ndiyo imekusanywa,” alisema.
“Hata kama Serikali itakusanya asilimia 100 kwa miezi yote iliyobaki hadi Juni 2017 bado lengo halitafikiwa kwa sababu kuna vyanzo Serikali imesema haitaweza kabisa ikiwamo mikopo ya kibiashara kutoka nje.”
Alisema Serikali imesema rasmi haitapata Sh trilioni 2 kutoka mikopo ya kibiashara, kwamba lengo la makusanyo litafikia asilimia 90 na hivyo kukosa Sh trilioni 1.7.
Alisema hata wafadhili wataongeza fedha hadi asilimia 80 (sasa wametoa asilimia 40 ya lengo), na hivyo kukosa Sh trilioni moja.
“Kwa hiyo Bajeti halisi itakuwa Sh trilioni 24.8 tu. Haya ni makisio ya juu kabisa na ni ongezeko linaloeleweka kulinganisha na bajeti ya Sh trilioni 22.9 aliyoiacha Saada Mkuya Salum (aliyekuwa Waziri wa Fedha) mwaka 2015/16,” alisema.
Alihoji sababu za Serikali kuleta Bajeti ya Sh trilioni 31.7 wakati Bajeti ya 2016/17 imeshindwa kufikiwa, “ Hili ndio swali kila mbunge makini anajiuliza hapa Dodoma. Serikali inataka kuzitoa wapi fedha za Bajeti mpya?”
Akifafanua kushindikana kutekelezwa kwa Bajeti hiyo, Zitto alisema mapato ya kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni Sh trilioni 17 kutoka Sh trilioni 15 za sasa ambazo hazitafikiwa kwa kiasi cha Sh trilioni 1.5, yaani asilimia 90 ya lengo la mwaka 2016/17.
“Mapato yasiyo ya kodi Sh trilioni 2.2 ambapo kwa sasa chanzo hiki kimefikia asilimia saba tu ya lengo la 2016/17. Mapato ya halmashauri ni Sh trilioni 0.7 ambapo kwa sasa chanzo hiki kimefikia asilimia 70 tu ya lengo la 2016/17,” alisema.
“Mikopo na misaada nafuu kutoka nje ni Sh trilioni 4 ambapo chanzo hiki kimefikia asilimia 40 tu ya lengo la 2016/17. Mikopo ya ndani na yenye masharti ya kibiashara ni Sh trilioni 8 ambapo chanzo hiki kimefikia asilimia 78 ya lengo la mwaka 2016/17.
from Blogger http://ift.tt/2oDRIzx
via IFTTT
from WordPress http://ift.tt/2nScImb
via IFTTT