TAARIFA KUHUSU ZIARA YA KATIBU MKUU WA CUF KISIWANI UNGUJA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU ZIARA YA KATIBU MKUU WA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama Cha Wananchi) KATIKA WILAYA ZA KISIWA CHA UNGUJA LEO TAREHE 08 FEBRUARI, 2017

Leo Jumatano, tarehe 08 Februari, 2017 Katibu Mkuu wa The Civic United Front (Chama Cha Wananchi), Maalim Seif Sharif Hamad, ameanza ziara ya siku nne katika Wilaya saba za Mikoa mitatu ya kisiwa cha Unguja.

Ziara hiyo iliyoanza asubuhi ya leo katika Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini-Unguja imelenga kukutana na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa chama na jumuiya zake kwa madhumuni ya kuhamasisha uhai wa chama na umuhimu wa viongozi hao kushiriki katika kutekeleza mikakati mbali mbali iliyoandaliwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF.

Baada ya kukamilika kwa ziara hiyo katika Wilaya ya Kusini, Katibu Mkuu alifanya mazungumzo na viongozi wa Chama Wilaya ya Kati Unguja ambapo katika msafara wa ziara yake aliambatana na viongozi wa Chama wa ngazi mbali mbali wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Mh. Nassor Ahmed Mazrui.

Wengine walioshiriki katika ziara hiyo ni Mkurugenzi wa Mipango na Chaguzi, Mh. Omar Ali Shehe, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Mh. Salim Bimani, na Naibu Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi, Mh. Abdalla Bakar Hassan.

Viongozi wengine waliokuwepo ni Naibu Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wanawake (JUKECUF), Mh. Zahra Ali Hamad, Kaimu Naibu Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wazee wa CUF (JUZECUF), Mh. Ali Abdallah Ali, viongozi wa Jumuiya ya Vijana wa CUF (JUVICUF) wakiongozwa na Makamo Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mh. Faki Suleyman Khatib na Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo Mh. Mahmoud Ali Mahinda.

Maalim Seif Sharif Hamad ataendelea na ziara yake katika Mikoa na Wilaya nyengine za Unguja kwa ratiba ifuatayo:

Asubuhi ya siku ya Alkhamis, tarehe 09 Februari, 2017 Katibu Mkuu atafanya ziara Mkoa wa Kaskazini Unguja na kuzungumza na viongozi wa chama na Jumuiya zake katika Wilaya ya Kaskazini ‘B’ na baadae mchana atafanya ziara na kuzungumza na viongozi wa chama na Jumuiya zake Wilaya ya Kaskazini ‘A’

Jumapili asubuhi, tarehe 12 Februari, 2017 ziara itafanyika Wilaya ya Magharibi ‘A’ na baadae mchana wa siku hiyo ziara itafanyika Magharibi ‘B’. Kwa upande wa Wilaya ya Mjini, ziara itafanyika Jumatatu tarehe 13 februari, 2017.

Baada ya kukamilika kwa ziara katika kisiwa cha Unguja, Katibu Mkuu na viongozi wenzake wataendelea na ziara katika kisiwa cha Pemba kuanzia tarehe 15 Februari hadi tarehe 24 Februari, 2017.

Pamoja na kufanya ziara na kuzungumza na viongozi wa chama na Jumuiya zake, Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad atafanya uzinduzi na uimarishaji wa waratibu wa chama, uzinduzi wa ofisi za chama na kuweka mawe ya msingi katika majengo ya chama katika maeneo mbali mbali ya kisiwa hicho.

Imetolewa na:
Hissham Abdukadir
Afisa Habari na Mawasiliano
The Civic United Front
CUF-Chama Cha Wananchi
Makao Makuu-Zanzibar




from Blogger http://ift.tt/2k66sZ6
via IFTTT




from WordPress http://ift.tt/2kuQHJS
via IFTTT