HATIMAYE ushahidi wa upande wa mshtakiwa katika kesi namba 6
ya uchaguzi mkuu ya mwaka 2015 nafasi ya ubunge jimbo la njombe mjini umefungwa
katika mahakama kuu kanda ya iringa kwa shahidi mmoja kutolea ushahidi kati ya
mashahidi wanne waliotajwa hapo awali.
Baada ya kukamilisha ushahidi huo katika kesi iliyofunguliwa
na Emmanuel Masonga aliyekuwa mgombea ubunge kupitia Chadema dhidi ya Edward Mwalongo
wa CCM ambaye alitangazwa kuwa mbunge wa jimbo la Njombe mjini, mahakama hiyo
imeanza kusikiliza mashahidi watatu wa upande wa serikali ambao hata hivyo
wanaendelea hapo kesho.
Aidha shahidi huyo wa mwisho kwa upande wa mshtakiwa Agnes
Mbanga mkazi wa Idundilanga mjini Njombe alitolea ushahidi namna mkutano wa
kampeni za ubunge wa chama cha mapinduzi zilivyokwenda hapo Oktoba 22 mwaka
2015 na kuwa Edwin Mwanzinga alieleza namna serikali ilivyofanyakazi ya kujenga
barabara ya lami ya magereza, ukarabati wa zahanati ya Idundilanga huku Edward Mwalongo akiahidi kuwasaidia
kutatua tatizo la maji, kuwasaidia vijana kujikwamua na wimbi la umasikini
pamoja na namna ambavyo anawasaidia watoto yatima.
Mara baada ya kukamilisha ushahidi huo wakili wa serikali
aliwaita mashahidi watatu kwa upande wa serikali ambao ni Venance Msungu
aliyekuwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi jimbo la Njombe mjini, Nelson Kyando
ambaye alikuwa mjumbe katika kamati ya maadili wakati wa kampeni pamoja na
William Myegeta ambaye alikuwa mmoja kati ya wagombea wanne wa ubunge katika
jimbo la Njombe mjini Kutoa ushahidi wao.
Katika hatua nyingine mashahidi hao watatu walieleza namna
ambavyo mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu ulivyokwenda na kwamba ulikuwa wa huru na haki katika kipindi chote
huku wengine wakikiri kuwa kulikuwa na mapingamizi ambayo hata hivyo tume
iliyashughulikia vizuri.
Jaji wa mahakama hiyo Jacob Mwambegele aliahirisha kesi hiyo
hadi kesho aprili 22 mwaka huu ambapo kesi hiyo inaendeshwa mfuruzizo bila
kupitisha siku na itakapoendelea kwa
mashahidi wa upande wa serikali.
Nje ya mahakama Nipashe ilizungumza na wakili wa Edward
Mwalongo upande wa mstakiwa Samson Rutebuka
kujua kwanini ameletwa shahidi mmoja pekee kati ya wanne walioelezwa hapo awali
alisema huyo mmoja amewakilisha kila kitu ambacho kilitakiwa kujibiwa
mahakamani hapo na kuwa hayo ni mambo ya kiufundi.
“Hiyo ndi mbinu ya kiufundi wa kisheria ambapo tumeona hoja
zote zilizo takiwa kujibiwa na na mashahidi wangu zimejibiwa kwa kuwa ilikuwa
ni lazima hoja zijibiwe lakini kwakuwa huyo mmoja amejibu kila kitu hakuna haja
ya kusababisha wengine kujakuendelea kueleza kilekile,” alisema Rutembuka.