Mmoja wa watu waliokuwa wamefunikwa na kifusi chini ya ardhi kwa siku 41, juzi jioni alizinduka na muda mfupi baadaye akaulizia kama aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa ameshinda Uchaguzi Mkuu.
Joseph Bulule ni mmoja kati ya wachimbaji watano waliokuwa wamefukiwa na kifusi kwenye machimbo ya Nyangalata wilayani Kahama tangu Oktoba 5, siku tatu baada ya Lowassa kurejesha fomu za kuwania urais kwa tiketi ya Chadema.
Juhudi za kuwaokoa wachimbaji hao zilifanyika lakini zikasitishwa baada ya muda kutokana na kutokuwapo na dalili za mafanikio, kabla ya jitihada hizo kuanza tena baada ya wachimbaji wengine kusikia sauti za wenzao wakiomba msaada kutoka chini ya ardhi.
Bulule, ambaye amelazwa Hospitali ya Halmashauri ya Kahama, aliuliza swali hiyo mbele ya waandishi wa habari baada ya kupata fahamu.
“Nani alishinda kwenye uchaguzi wa Rais,” aliuliza waandishi akiwa amelala kitandani. “Lowassa alishinda? Maana sisi tangu Oktoba 5, tulipofukiwa hatujui kinachoendelea. Uchaguzi umetukuta ndani ya mashimo na hatujui matokeo ya uchaguzi.”
Uchaguzi wa Rais na wabunge ulifanyika siku ishirini baadaye wakati juhudi za kuwaokoa zikiwa zimeshasitishwa. Katika matokeo ya uchaguzi huo, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli alishinda kwa kupata kura milioni 8.88, huku Lowassa, aliyekuwa anaungwa mkono na vyama vinne, akishika nafasi ya pili kwa kupata kura milioni 6.07
Baada ya waandishi wa habari kumueleza kuwa aliyeshinda ni Dk Magufuli, mchimbaji madini huyo mdogo alionekana kukosa raha.
Kwa mujibu wa mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Joseph Ngowi jana mchana watu hao watano walianza kupatiwa chakula chepesi, kama uji wenye maji mengi ambayo alisema yanasaidia utumbo kunyanyuka baada ya kukaa siku 41 bila kupata chakula.
Alisema baada ya hatua hiyo wataanza kupewa chakula laini na baada ya siku saba wataanzza kula chakula cha kawaida. Alisema wote watano wapo kwenye usimamizi wa madaktari pamoja na wataalamu.
Wakiwa kwenye mgodi Oktoba 5, kifusi kilikatika na kufunika mlango wa kutokea, hali iliyofanya waishi siku 41 kwa kunywa maji, kula mende, vyura na magamba ya miti hadi walipookolewa Jumapili iliyopita wakiwa hai.