Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita ametangaza hali ya hatari nchini humo baada ya shambulio kwenye hoteli moja mjini Bamako kuua watu zaidi ya 20.
Bw keita ametangaza hali ya hatari itakayodumu kwa siku 10, pamoja na siku tatu za maombolezo ya kitaifa.
Watu wenye silaha wanaodaiwa kuwa wanamgambo wa kundi la Kiislamu walishambulia hoteli ya Radissom Blue mjini Bamako na kushikilia mateka watu 170.
Maafisa wa Marekani wamethibitisha hakuna mateka zaidi wanaoshikiliwa.
Makundi ya Al-Qaeda Afrika Kaskazini na kundi jingine la al-Murabitoun yamedai kuhusika kwenye shambulio hilo.
Baraza kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshutumu shambulio hilo.
Akiongea baada ya mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri, Rais Keita alisema watu 21 waliuawa kwenye shambulio hilo, wakiwemo washambuliaji wawili.
Ripoti za awali zilikuwa zimesema watu 27 waliuawa. Afisa wa UN, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema miili 12 ilipatikana ghorofa ya chini ya hoteli hiyo na miili 15 ghorofa ya pili.
Mmoja wa mateka waliouawa ni Geoffrey Dieudonne, mbunge aliyewakilisha jimbo la Wallonia nchini Ubelgiji.
Shirika la habari la serikali ya Uchina Xinhua linasema raia watatu wa Uchina ni miongoni mwa waliouawa. Marekani nayo ilisema raia wake mmoja aliuawa.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza Philip Hammond alisema Waingereza watatu waliokuwa hotelini humo wako salama.
Hoteli hiyo inamilikiwa na Wamarekani na hupendwa sana na raia wa kigeni.
Watu walioshuhudia shambulio hilo walisema wapiganaji hadi 13 waliingia kwenye hoteli hiyo wakiimba "Mungu ni Mkubwa!” kwa Kiarabu.
Kabla ya vikosi maalum kuingia humo, mdokezi mmoja aliambia shirika la habari la Reuters kwamba baadhi ya mateka walioweza kukariri vifungu vya Koran waliachiliwa.