Na Mwandishi Maalum – Maelezo
Vyombo vya habari nchini vimepongezwa kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kutoa taarifa kwa wananchi wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwezi wa 10 mwaka huu.
Pongezi hizo zimetolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akiongea na viongozi wa menejimenti ya wizara na taasisi zake kwenye kikao cha kazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Prof. Gabriel alisema kipindi cha uchaguzi vyombo vya habari vilifaya kazi kubwa ya kuwahabarisha wananchi habari za uchaguzi kwa kuzingatia weledi wa taaluma yao na hivyo kuwawezesha wananchi kujua mambo mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea hapa nchini.
Katibu Mkuu huyo ambaye hicho kilikuwa ni kikao chake cha kwanza tangu ateuliwe kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo mwishoni mwa mwezi wa kumi aliahidi kuwatumikia na kuwaheshimu wafanyakazi wa wizara yake huku akisimamia majukumu ya kazi kwa kufauata kanuni, taratibu na sheria za utumishi wa Umma.
“Hiki ni kikao chetu cha kujipanga kwa ajili ya kazi, ni vyema tukajipanga huku tukijuwa matarajio ya Mhe. Rais kwetu ni yapi, wananchi tunaowatumikia wanategemea kupata nini kutoka kwetu na mimi kama Katibu Mkuu natarajia kupata nini kutoka kwenu”, Prof. Gabriel alisema.