Zanzibar. Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema yuko tayari kukamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka, kama kitendo chake cha kujitangazia ushindi ni kosa.
Maalim Seif alikuwa akizungumza na viongozi wa majimbo, makatibu wa matawi, wajumbe wa mkutano mkuu, wajumbe wa kamati za utendaji za ngazi zote na watendaji wa chama hicho.
Alisema haoni hatua yake ya kuitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imtangaze kuwa mshindi haina matatizo kwa kuwa ana uhakika kuwa ndiye aliyeshinda kwenye uchaguzi.
“Nilichosema ni ZEC initangaze kwa kuwa nilishinda uchaguzi. Je, hapo kuna ubaya gani ati? Nishitakini basi, nasema niko tayari, nishtakini. Nitakuja mahakamani kujitetea, mnamtisha nani! Mnamtisha nani hapa?” alihoji.
Maalim Seif aliwania urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), akichuana vikali na mgombea wa CCM, Dk Mohamed Shein.
Hadi sasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) haijamtangaza mshindi na badala yake imefuta matokeo ya kura za nafasi hiyo pamoja na za uchaguzi wa wawakilishi, ikisema uchaguzi utarudiwa tena ndani ya siku 90.
Hata hivyo, CUF imepinga ikitaka ZEC imtangaze mshindi kwa madai kuwa chama hicho ndicho kilichoibuka na ushindi.
Jana, Maalim Seif, ambaye ameshagombea urais wa Zanzibar mara tano, alirudia wito wake wa kuitaka ZEC imtangaze kuwa mshindi ili aapishwe na kuanza kazi, ikidai anataka kuanza kuijenga upya Zanzibar. Pia alisisitiza msimamo wake wa kushirikiana na CCM katika utawala wake kwa kuwa Katiba ya Zanzibar inaelekeza chama kinachoshinda kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
“Sijui wenzetu wanachohofia ni nini na mara hii sisi (CUF) tumeshinda viti 27 na wao idadi hiyo hiyo ya viti 27 vya Baraza la Wawakilishi, tutakuwa na idadi sawa kwa sawa ya mawaziri tuongoze nchi pamoja,” alisema Maalim Seif.
Kiongozi huyo wa CUF alihoji sababu za Rais Shein kutokubali kushindwa akihoji anaona ubaya gani kuridhia.
“Tukae pamoja tuunde Serikali akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais au kama hataki CCM wamteue mtu yoyote tuongoze nchi. Mbona mimi niliridhia kuwa Makamu wa Kwanza?” alihoji.
Maalim Seif alisema hakuna namna yoyote ya kupindua uamuzi wa wananchi walioufanya kupitia masanduku ya kura.
Alisema wanachokifanya ZEC ni kuchelewesha kukamilisha uhakiki wa kura kwa majimbo 14 yaliyobakia na kumtangaza mshindi wa urais, na hivyo kuishauri ZEC kukamilisha kazi ili serikali mpya ianze kufanya kazi ya watumikia wananchi.
Alisema tayari dunia nzima wanamfahamu rais aliyechaguliwa na wananchi wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu uliopita, na kuwataka wanachama wa CUF kuacha kusikiliza kile alichokiita proganda za CCM zinazoeleza kurejewa kwa uchaguzi.
Akizungumzia madai ya ongezeko la kura katika kisiwa cha Pemba, Maalim Seif alisema hayo hayana ukweli kwani hakuna hata ‘kituo kimoja kilichozidishwa wapiga kura 350 kama ZEC ilivyopanga, akisema vingine vilikuwa na wapigakura chini ya idadi hiyo.
Mapema akizungumza katika mkutano huo, mkurugenzi wa mipango na uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe alisema chama hicho kimepata ushindi mkubwa kwa nafasi za uwakilishi na udiwani.
Alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 chama hicho kilipata wawakilishi wanne na madiwani saba kisiwani Unguja, lakini katika uchaguzi wa 2015 kimepata wawakilishi tisa na madiwani 15.
Kiongozi huyo alisema CCM imepoteza kata zote tatu za udiwani katika kisiwa cha Pemba na kukifanya chama hicho kushindwa kupata mjumbe katika Baraza la Wawakilishi, ubunge na udiwani.
Kabla ya mkutano huo, alielezea kauli ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la CUF kilichokutana chini ya mwenyekiti wake, Twaha Taslima, akisema kiliishauri ZEC kutengua uamuzi wa mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha wa kufuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar, kwa vile hana mamlaka ya kikatiba na wala Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar hampi nguvu ya kufuta uchaguzi huo.
Jecha amekuwa akidaiwa kufanya uamuzi huo bila ya kushirikisha viongozi wenzake wa ZEC.
Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanatakiwa kutolewa siku tatu baada ya wananchi kupiga kura na yanaweza kucheleweshwa kwa siku tatu zaidi iwapo kutatokea matatizo katika kuhesabu kura.