KATIKA kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya nchini umetoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya sh.milioni tano kwa Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo inalenga kuongeza jitihada za kukabiliana na ugonjwa huo ambao umekuwa ukienea kwa kasi, tangu uanze Agosti 15, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mara baada ya kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa Fedha, Mipango na Uwekezaji wa mfuko huo, Deusdedit Rutazaa alisema kutokana na kuguswa na mwenendo wa ugonjwa huo jijini Dar es Salaam ndio maana wametoa msaada huo.
Alisema hiyo ni hatua ya awali waliyoianza kwa ajili ya kutokomeza na kukabiliana na ugonjwa huo ambao umesababisha vifo vya watu 18, huku takribani watu 200 wamekumbwa na ugonjwa huo.
“Katika msaada huo tumekabidhi boksi za Gloves za mikononi, dawa za kuwa vimelea na bacteria pamoja na dawa za maji, hivyo tunaimani kwa hatua hii tuliyoichukua tutaweza kudhibiti na kutokomeza kabisa,”alisema.
Pia Rutazaa aliongeza kuwa katika uthaminifu wa afya wameanza mpango wa kutoa mikopo ya Hospitali na Zahanati mbalimbali kwa ajili ya kujiendesha zenyewe kitabibu ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Tiafa Muhimbili.
“Mikopo tutayotoa itahusisha hadi kwenye masuala ya dawa ambapo mgonjwa atapatiwa katika eneo husika na kupata tiba sahihi,”alisema.
Kwa upane wake, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Mussa Natty alisema kuwa msaada huo utasambazwa kwenye kambi mbalimbali za wagonjwa wa kipindupindu ili kuboresha huduma.
Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF), Athumani Rehani akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya sh.milioni Tano kwa Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Fedha, Mipango na Uwekezaji kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Deusdedit Rutazaa akisisitiza jambo katika hafla hiyo.
Mkurugenzi wa Fedha, Mipango na Uwekezaji wa NHIF, Deusdedit Rutazaa (kushoto) akikabidhi msaada wa vifaa tiba kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Mussa Natty (kulia), jijini Dar es salaam leo. Katikati ni Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF), Athumani Rehani.
Sehemu ya wadau mbalimbali waliofika kwenye hafla hiyo leo. Picha na Emmanuel Massaka.