Mhe. Mahadhi J. Maalim Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akizungumza wakati wa Mkutano wa Nchi zilizonyuma kimaendeleo ( LDCs) wakati wa mkutano wa Mawaziri wa Kundi hilo uliofanyia siku ya Alhamis hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Nyuma ya Naibu Waziri, ni Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan M. Mwinyu
Na Mwandishi Maalum, New York
Wakati kila Nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, ikijianda kwa utekelezaji wa Ajenda 2030 ambayo inajikita zaidi katika kuondoa umaskini pasipo kumwacha yeyote nyuma, sanjari na kuilinda Sayari Dunia. Tanzania imehimiza haja na umuhimu wa nchi ambazo ziko nyuma kimaendeleo ( LDCs) kuzungumza kwa kauli moja.
Ushauri huo umetolewa jana Alhamis na Mhe. Mahadhi Juma Maalim ( Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wakati akizungumza katika mkutano wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa LDCs uliofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, sambamba na majadiliano ya jumla ya Mkutano wa 70 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Katika mkutano huu wa Mawaziri wa LDCs, Bangladesh ilikabidhiwa uenyekiti wa Kundi hilo kutoka kwa Benin inayomaliza muda wake. Pamoja na Kuishukuru Benin kwa kuliongoza kundi hilo vema wakati wa uenyekiti wake Mhe. Naibu Waziri ameiahidi Bangladesh ushirikiano kutoka Tanzania.
“
Kundi letu linawachama wengi, tutumie basi wingi wetu kuhakikisha kwamba tunasukuma mbele na kuteteta masuala yanayotuhusu kwa kuzungumza kwa sauti moja wakati wa majadiliano na kuhakikisha kuwa ajenda tunazosimamia kwa maslahi yetu hazikwami.” Amesema Naibu Waziri
Aidha Naibu Waziri Mahadhi, amelikumbusha kundi hilo kuwa moja ya lengo kuu la kundi ni kuondoka katika kundi la nchi maskini na kuwa nchi zenye uchumi wa kati.
“ Kwa bahati nzuri suala la kuondoa umaskini ni moja ya eneo ambalo limepewa umuhimu wa kipekee katika Ajenda 2030, hivyo ni wajibu wetu kama LDCs, kutumia fursa hii kwa kuhakikisha kwamba, katika kipindi cha miaka 15 ijayo nchi nyingi katika kundi letu zina-graduate na kuwa nchi zenye uchumi wa kati”. Amesisitiza.
Mhe. Naibu Waziri amerejea kwa kusisitiza kauli iliyotolewa na Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipolihutubia Baraza Kuu la 70 la Umoja wa Mataifa, siku ya Jumanne, Kwamba utekelezaji wa Ajenda 2030 ndiyo changamoto iliyombele yetu kwa sasa na kwamba utekelezaji wake ukikwama, LDCs ndizo zitakazo athirika zaidi.
Ni kwa sababu hiyo juhudi za pamoja katika kuhakikisha utekelezaji wa Ajenda 2030 ni mihimu na za lazima.
Kundi la Nchi ambazo zipo nyuma kimaendeleo na kama zinavyotambuliwa na Umoja wa Mataifa zipo 48
Ajenda 2030 ambayo ilipitishwa wakati wa mkutano wa kilele wa kisiasa uliofanyia kwa siku tatu hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, ni Ajenda yenye malengo 17 ya maendeleo endelevu yakichukua na nafasi ya Malengo ya Maendeleo ya Milenia ambayo yanafikia ukingoni mwaka huu wa 2015
Ajenda 2030 itaanza kutekelezwa mwakani ( 2016 )na utekelezaji wake ni wa miaka 15