JK akumbushwa kutangaza mali alizochuma kabla ya kung'atuka.

Mkurugenzi wa Idara ya Utetezi na Maboresho kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia, amemkumbusha Rais Jakaya Kikwete, asiondoke kimyakimya bila kutangaza au kuorodhesha mali alizochuma wakati akiwa madarakani.

“Rais Kikwete alijaza fomu ya mali alizokuwa nazo Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, lakini hakutangaza. Tunasubiri kuona sasa baada ya kumaliza atatangaza mali aliyopata akiwa madarakani,” alisema.

Alisema mwaka 1995, Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, alipoingia madarakani alitangaza mali zake, lakini alipong’atuka, ‘alisahau’ kutangaza, pengine ni kutokana na majukumu aliyokuwa nayo kitaifa sasa tunasubiri kuona kwa Rais Kikwete,” alisema. Kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13, 1995 na kanuni zake, mwananchi anaweza kupata taarifa za mali za viongozi kwa kufuata utaratibu uliopo, lakini baada ya kupata taarifa hizo, haruhusiwi kuzitangaza au kuzichapisha kwenye vyombo vya habari. 

Hoja hiyo iliibuka katika semina ya mafunzo kwa washiriki 103 yaliyoandaliwa na asasi ya HakiKazi Catalyst ya jijini hapa, kuhusu ‘Maadili ya viongozi na watumishi wa umma katika usimamizi wa rasilimali: Ipi nafasi ya wananchi kuhimiza na kuchochea uwajibikaji?’ Washiriki wa mafunzo hayo walikuwa ni maofisa watendaji wa kata, mitaa pamoja na wenyeviti wa mitaa na vijiji, wawakilishi wa vyama vya siasa, viongozi wa mila, wenyeviti wa ufuatiliaji wa rasilimali za jamii (Sedla) kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

Aliwafundisha washiriki hao kuhusu misingi ya maadili ya viongozi wa umma kama vile kufanya kazi kwa uaminifu na huruma, kujizuia na tamaa na kujiheshimu, kujituma na kutekeleza majukumu kwa umahiri na kufanya kazi bila upendeleo. Misingi mingine ni kutoa tamko la rasilimali na madeni, kuepuka mgongano wa kimaslahi, suala ambalo ndilo limelifikisha taifa hapa lilipo na kuepuka kupokea zawadi, fadhila au maslahi ya kiuchumi yaliyokatazwa. Lengo la semina hiyo ilikuwa ni kuwawezesha wananchi kupata ufahamu mpana wa maadili ya viongozi wa umma na nafasi ya wananchi kuhimiza na kuchochea uwajibikaji.
CHANZO: NIPASHE